Habari

WAJUMBE WAPYA WA BARAZA LA ARDHI TUNDURU WAHIMIZWA KUWA WAADILIFU NA KUTENDA HAKI

  • 21 Sep, 2026
WAJUMBE WAPYA WA BARAZA LA ARDHI TUNDURU WAHIMIZWA KUWA WAADILIFU NA KUTENDA HAKI

Wajumbe wanne wameapishwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, kuwa Wajumbe wapya wa Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Tunduru, ikiwa ni hatua ya kuimarisha upatikanaji wa haki na utatuzi wa migogoro ya ardhi na nyumba wilayani humo.

 

Zoezi hilo limefanyika leo, Septemba 18, 2026, ambapo wajumbe hao wamekula Kiapo cha Uaminifu pamoja na Kiapo cha Kutekeleza Majukumu yao mbele ya Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Mhe. Brigedia Jenerali Ahmed Abbas na kuahidi kutekeleza dhamana waliyopewa kwa kuzingatia sheria, haki, uadilifu na maslahi ya wananchi.

 

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Abbas, amewataka wajumbe hao kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, weledi na bila upendeleo huku akisisitiza umuhimu wa kuzingatia sheria na ushahidi katika kushughulikia migogoro ya ardhi na nyumba.

 

Amesema nafasi waliyopewa ni dhamana kubwa kwa wananchi, hivyo wanapaswa kusikiliza kwa umakini pande zote zinazohusika katika migogoro na kuhakikisha haki inatendeka kwa wakati.

 

Mkuu huyo wa Mkoa wa Ruvum pia amewataka wajumbe hao kufanya kazi kwa weledi na uwajibikaji ili kusaidia kupunguza migogoro ya ardhi na nyumba, pamoja na kujenga imani ya wananchi katika mifumo ya utoaji haki.

 

Uapisho wa wajumbe hao ni sehemu ya jitihada za kuimarisha mifumo ya utoaji haki na kuhakikisha wananchi wanapata huduma za utatuzi wa migogoro ya ardhi kwa ufanisi, haki na kwa kuzingatia misingi ya sheria.

 

Hatua hiyo pia inatarajiwa kuongeza ufanisi katika utendaji wa Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Tunduru na kuwezesha wananchi kupata huduma za utatuzi wa migogoro kwa wakati, huku haki za pande zote zikizingatiwa.