Habari

VIWANJA 4,150 VYAMILIKISHWA KUPITIA PROGRAMU YA UKWAMUAJI URASIMISHAJI DAR ES SALAAM

  • 02 Jul, 2024
VIWANJA 4,150 VYAMILIKISHWA KUPITIA PROGRAMU YA UKWAMUAJI URASIMISHAJI DAR ES SALAAM

Jumla ya viwanja 4,150 vimemilikishwa katika mitaa 270 ya mkoa wa Dar es salaam kupitia programu ya ukwamuaji urasimishaji pamoja na klinik ya ardhi katika kipindi cha kuanzia januari hadi Machi 2024.

 

Aidha, programu hiyo imewezesha viwanja 55,034 kupangwa na vingine 6,824 kupimwa sambamba na elimu kutolewa kwa kamati za urasimishaji za mitaa 46 ambapo jumla ya viwanja 2,727 vinavyotakiwa kumilikishwa vimeibuliwa.

 

Hayo yamebainishwa leo tarehe 1 Julai 2024 mkoani Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii ilipopokea taarifa ya utekelezaji zoezi la ukwamuaji urasimishaji katika jimbo la Ukonga Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam.

 

Kwa mujibu wa Mhe. Pinda, miradi ya urasimishaji katika halmashauri za mkoa wa Dar es Salaam ilianza kutekelezwa mwaka 2013 ambapo hadi kufikia mwezi Desemba 2023 jumla ya viwanja 565,690 vilikuwa vimepangwa ambapo viwanja 132,811 vilipimwa na viwanja 42,513 vilimilikishwa.

 

"Takwimu hizi zinaonesha kuwa, utekelezaji wa programu ya urasimishaji wa makazi yasiyopangwa ulikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kasi ndogo ya upimaji na umilikishaji wa viwanja vilivyopangwa" alisema Mhe. Pinda. 

 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii Mhe. Timotheo Mzava ameishukuru serikali kwa kuwezesha ukwamuaji urasimishaji maeneo ya makazi holela kupitia Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki (LTIP) hasa ikizingatiwa zoezi hilo halikwenda vizuri siku za nyuma.

 

"Wenzetu wa wizara ya Ardhi wamefanya vizuri sana katika zoezi la ukwamuaji urasimishaji lakini niwatake wananchi kutoa ushirikiano wakati wa utekekezaji zoezi hilo na kwa upande wa wizara waongeze  kasi ya utekelezaji zoezi ili wananchi waweze kumilikishwa kwa hati" alisema Mhe. Mzava

 

Katika ziara yake, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii ilipokea taarifa ya utekelezaji zoezi la ukwamuaji kazi za urasimishaji katika mkoa wa Dar es Salaam, kuongea na kamati za urasimishaji za manispaa ya ilala pamoja na kugawa hati milki za ardhi kwa wananchi. Aidha, katika siku yake ya kwanza ya ziara yake jijini Dar es Salaam, kamati hiyo ilikagua miradi inayotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC)