Habari

VIWANJA 2,618 VYAPIMWA HALMASHAURI YA MJI WA MAFINGA

  • 17 Sep, 2025
VIWANJA 2,618 VYAPIMWA HALMASHAURI YA MJI WA MAFINGA

Jumla ya viwanja 2,618 kati ya 7,445 vilivyopangwa katika kata ya Upendo na Kinyanabo Halmashauri ya Mji wa Mafinga mkoa wa Iringa vimepimwa baada ya kazi ya upangaji kukamilika.

Hayo yameelezwa tarehe 16 Sept 2025 na kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Iringa Bi. Rehema Kilonzi wakati wa zoezi la Klinik ya Ardhi linaloendelea katika kata ya Upendo ndani ya Halmashauri ya Mji wa Mafinga.

Amesema, kukamilika kwa upimaji viwanja 2,618 katika kata hizo kumeifanya ofisi yake kuandaa klinik ya ardhi kwa ajili ya kukamilisha zoezi la umilikishaji wananchi ambao maeneo yao tayari yamefanyiwa upimaji.

''Tunashukuru muitikio wa wananchi ni mzuri kuanzia siku ya kwanza ya zoezi la klinik ya ardhi hapa katika kata ya Upendo na nitoe wito kwa wananchi wa kata ya Upendo kujitokeza kwa wingi na kuchangamkia fursa ya kumilikishwa ardhi ya maeneo yao'' amesema Bi. Rehema Kilonzi.

Baadhi ya wananchi waliofika kupata huduma katika klinik hiyo ya ardhi, wamesema zoezi hilo ni zuri kwa kuwa limewafuata wananchi katika maeneo yao na kuelezea kuwa, klink hiyo ya ardhi inawarahisishia kupata huduma kwa ukaribu zaidi na haraka.

''Nimetumia takriban dakika 20 kuanzia kupokelewa, kupatiwa ankara ya malipo na kuandaliwa nyaraka, nimepigiwa tu simu nije hapa na sikudhani kama itakuwa haraka kiasi hiki nimeshangaa kweli na natamani huduma hii itolewe katika kata zote''.

''Naipongeza sana serikali kwa kuamua kuwafuata wananchi hadi katika ngazi ya kata na kutoa huduma za ardhi '' amesema mwananchi aliyenufaika na huduma ya klinik ya ardhi katika kata ya Upendo Bw. Godfrey Mduda.

Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imekuwa ikiendesha Klinik za Ardhi maeneo mbalimbali nchini lengo likiwa kusogeza huduma karibu na wananchi. Kupitia Klinik hizo huduma mbalimbali zimekuwa zikitolewa kama vile utoaji hati milki za ardhi papo hapo, kusikiliza na kutatua changamoto za ardhi, kutoa ushauri wa masuala ya ardhi, kukadiria kodi ya pango la ardhi pamoja na kutoa elimu juu ya sheria ya ardhi.