Habari

VIONGOZI PELEKENI TAARIFA SAHIHI KWA WANANCHI

  • 27 Jun, 2024
VIONGOZI PELEKENI TAARIFA SAHIHI KWA WANANCHI

Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Mhe. Beno Malisa amewaagiza viongozi katika Wilaya hiyo kutoa elimu sahihi kwa wananchi juu ya utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) unaotekelezwa chini ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

 

Malisa ameyasema hayo tarehe 20 Juni 2024 wakati wa ufunguzi wa kikao cha kujadili utekelezaji wa mradi wa LTIP katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya.

 

‘‘Lengo la kufanya mikutano hii ni kuwa na uelewa wa pamoja kabla ya kwenda kukutana na wananchi ili wahusika waelewe vizuri mradi huu na kusiwe na kikwazo katika utekelezaji wake. Katika mkutano huu kuna wadau mbalimbali kama Madiwani, Wazee maarufu, Viongozi wa Dini hivyo tumieni nafasi zenu katika kutoa taarifa sahihi juu ya mradi huu ili wananchi wakauelewe’’ amesema Malisa.

 

Aidha, Malisa amesema mradi wa LTIP utarasimisha makazi yasiyorasmi kwa kutambua, kupanga, kupima na kumilikisha viwanja visivyopungua 29,014 katika mitaa 44 katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya.

 

Mstahiki Meya wa Jiji la Mbeya Mhe. Dormohamed Issa Rahmat amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mradi huu utakaotatua migogoro ya ardhi katika maeneo yao na kuwaomba watendaji wote kutoa ushirikiano wa kutosha katika utekelezaji wa mradi na kufikisha ujumbe wa mkutano huu kwa wananchi katika maeneo yao.  

 

Nae Meneja Urasimishaji Mjini katika Mradi wa LTIP Bw. Leons Mwenda amesema kuwa kazi ya utoaji elimu juu ya utekelezaji wa mradi huu inafanywa kwa kuwashirikisha asasi za kiraia pamoja na maafisa maendeleo wa Kata ambapo hupata nafasi ya kuzunguka nyumba kwa nyumba na kutoa elimu ya masuala ya ardhi.

 

‘‘Kutoa elimu kwa wananchi kumekuwa na mafanikio makubwa kwa kuwa hata asilimia ya umiliki wa ardhi kwa wanawake imeongezeka pamoja na umiliki wa ardhi wa pamoja ambapo kutokana na mafanikio hayo bidii zaidi inaendelea kuwekwa ili kufikia watanzania wengi zaidi ili kutambua Sheria na Taratibu katika umiliki wa ardhi’’ amesema Mwenda.

 

Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi una lengo kuu la kuboresha usalama wa milki za ardhi kwa kuwahusisha wadau katika kila hatua ya utekelezaji wake ili kuwe na uelewa wa pamoja.