Habari
VIJANA KUSHIRIKI USANIFU WA MIJI NCHINI
- 01 Sep, 2026
Serikali imesema itaendelea kushirikisha makundi yote ya wadau, likiwemo kundi la vijana, katika mipango na uendelezaji wa miji nchini ili kuhakikisha kuwa ujenzi wa miji unakuwa wa kisasa, unaostahimilika na endelevu.
Kauli hiyo imetolewa leo tarehe 31 Agosti 2026 Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Kaspar Mmuya, wakati akijibu swali la mbunge wa jimbo la Nungwi Mhe. Mdowe Haji Kombo.
Mhe. Mmuya ameeleza kuwa serikali inatambua mchango mkubwa wa vijana katika ujenzi wa miji ya kisasa. Ili kufanikisha hilo, serikali imeweka misingi thabiti ya kisera na kisheria, ikiwa ni pamoja na Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995 (Toleo la 2023), Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Makazi ya mwaka 2000, pamoja na Sheria ya Mipangomiji (Sura ya 355).
Sheria na sera hizo zinasitiza ushirikishwaji wa jamii, utumiaji endelevu wa ardhi, na uhusishaji wa wadau wote katika maendeleo ya miji.
Amesisitiza kuwa ushiriki wa vijana ambao ni takribani asilimia 35 ya watu wote nchini ni nguzo muhimu sana katika upangaji wa miji ili kufikia Lengo namba 11 la Maendeleo Endelevu (SDG 11) pamoja na Agenda Mpya ya Miji (New Urban Agenda) ya mwaka 2016 - 2036.