Habari

URASIMISHAJI KUMALIZA MIGOGORO YA ARDHI DAR ES SALAAM

  • 22 Feb, 2024
URASIMISHAJI KUMALIZA MIGOGORO YA ARDHI DAR ES SALAAM

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Jerry Silaa amesema Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetenga fedha kwa ajili ya kukwamua urasimishaji katika mkoa wa Dar es salaam ili kumaliza migogoro ya ardhi katika mkoa huo.

Waziri Silaa amesema hayo Februari 20, 2024 wakati wa akizindua Kliniki ya Ardhi inayoendelea katika viwanja vya shule ya msingi Bunju A  jijini Dar es salaam ambapo ambapo Pamoja na kutatua migogoro ya ardhi, wananchi pia wanakabidhiwa hati za umiliki wa ardhi wanayotumia kwa shughuli mbalimbali za maendeleo.

"Na hivi ninavyozungumza, tayari nimemteua Mratibu wa Urasimishaji Mkoa wa Dar es salaam Bw. Paul Mbembela, huyu ndiye Mratibu wa Urasimishaji mkoa huu, tunataka kufikia tarehe 30 mwezi Juni 2024 urasimishaji wote mkoa wa Dar es salaam uwe umekamilika katika wilaya zote za Kigamboni, Kinondoni, Ilala, Temeke na Ubungo" amesema Waziri Silaa.

Aidha, Waziri Silaa amesema kutakuwa na kikao cha urasimishaji hivi karibuni ambacho kitawahusisha wataalam wa wizara, waratibu wote urasimishaji katika wilaya za mkoa wa Dar es salaam, Wabunge, madiwani na wenyeviti wa mitaa ili kila mtu anapotoka katika kikao hicho aondoke na majibu kwa kuwa ukwamuaji wa ardhi katika mkoa huo.

Akitolea mfano, Waziri Silaa ameongeza kuwa kakao hicho kitaangalia ni mitaa mingapi imekwama katika wilaya Kinondoni, wataangalia mitaa ya ambayo wataifanyia sampuri na wataanza ukwamuaji wa urasimishaji wa ardhi ili kutekeleza maelekezo waliyopewa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutatua migogoro ya ardhi kwa wananchi nchini.