Habari
UHAKIKI TAARIFA ZA VIPANDE VYA ARDHI NA MALI MAKANGIRA WAANZA
- 22 Jun, 2026
Wananchi wa Mtaa wa Makangira, Kata ya Msasani jijini Dar es Salaam wameanza kuhakiki taarifa za vipande vya ardhi na mali zao kwa lengo la kuhakikisha usahihi wa taarifa zitakazotumika katika utekelezaji wa Mradi wa Uendelezaji wa Mji wa Makangira unaosimamiwa na Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Zoezi hilo litakalofanyika kwa siku 10 linafuatia mkutano wa hadhara uliofanyika Juni 20, 2026 katika Ofisi ya Serikali ya Mtaa wa Makangira, ambapo wananchi walipatiwa elimu kuhusu malengo ya mradi huo, umuhimu wa uhakiki wa taarifa za vpande vya Ardhi na wajibu wao katika kufanikisha utekelezaji wa mradi huo wa kimkakati.
Akizungumza katika mkutano huo, Afisa Mipango Miji Mwandamizi kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bw. Martin Orden Mwitula aliwataka wananchi kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo kwa kuhakiki taarifa zao kwa umakini na kutoa ushirikiano kwa wataalamu wanaotekeleza shughuli hiyo.
Amesema lengo la uhakiki wa Vipande vya ardhi na mali katika eneo hilo ni kuziboresha kwa kufanya marekebisho kwa kushirikiana na wataalamu ili ziakisi hali halisi kwa sababau zitatumika wakati wa uandaaji na utekelezaji wa mradi wa eneo la Makangira unaosimamiwa na Serikali kupitia Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Bw Martini,Amesema usahihi wa taarifa za vipande vya ardhi na Mali ni msingi muhimu wa utekelezaji wa mradi huo, akisisitiza kuwa wananchi watakaobaini makosa au upungufu katika taarifa zao wanapaswa kutoa taarifa mapema ili marekebisho yafanyike kwa wakati na kuhakikisha haki za kila mmiliki wa kiwanja zinalindwa.
Mkutano huo ulihudhuriwa na zaidi ya wananchi 400 kutoka matawi 12 ya Mtaa wa Makangira na uliongozwa na Mwenyekiti wa Mtaa wa Makangira, Bi. Daima Ally Issa, pamoja na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya mradi wa Maboresho ya Maendeleo ya Makangira, Bi. Janet Mmari, ambao waliwahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki katika zoezi hilo muhimu linalolenga kupanga mustakabali bora wa eneo lao.
Viongozi hao walieleza kuwa ushiriki wa wananchi katika uhakiki wa taarifa ni hatua muhimu ya kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa uwazi, usawa na kwa kuzingatia maslahi ya wakazi wote wa Makangira.
Mradi wa Uendelezaji wa Mji wa Makangira ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuboresha makazi, miundombinu na mazingira ya miji ili kuendana na kasi ya ukuaji wa miji na mahitaji ya maendeleo ya wananchi. Kupitia mradi huo, Serikali inatarajia kuvutia uwekezaji, kuongeza thamani ya ardhi, kuimarisha huduma za kijamii na kiuchumi pamoja na kuweka mazingira bora ya makazi ya kisasa.
Utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kuibadilisha Makangira kuwa kitovu na kichocheo cha uchumi kwa maendeleo ya kisasa , miundombinu bora, majengo ya kisasa na mazingira salama ya kuishi hatua ambayo itachangia kukuza uchumi wa Jiji la Dar es Salaam na kuongeza ustawi wa wananchi wa eneo hilo.