Habari

TUMIENI FURSA YA BAJETI KUPANGA MATUMIZI YA ARDHI VIJIJI VILIVYOBAKI KUDHIBITI MIGOGORO YA ARDHI

  • 08 Sep, 2026
TUMIENI FURSA YA BAJETI KUPANGA MATUMIZI YA ARDHI VIJIJI VILIVYOBAKI KUDHIBITI MIGOGORO YA ARDHI

Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) imetakiwa kutumia Bajeti ya mwaka 2026/27 kuwa kichocheo cha kuhakikisha Vijiji vyote nchini vinaandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi.

 

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe Kaspar Kaspar Mmuya Septemba 7, 2026 ametoa kauli hiyo wakati wa ziara yake katika Ofisi za Tume hiyo ambapo alipata fursa ya kuzungumza na Menejimenti pamoja na watumishi wa Tume kuhusu utekelezaji wa majukumu yake, mafanikio yaliyopatikana na hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili kuongeza kasi ya upangaji wa matumizi ya ardhi nchini.

 

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Mhe. Mmuya ameipongeza Tume kwa kazi kubwa inayotekelezwa katika kipindi cha Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, hususan katika kuhakikisha Vijiji vyote nchini vinaandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi.

 

Amesema Serikali imeendelea kuonesha dhamira ya dhati ya kutatua changamoto za migogoro ya matumizi ya ardhi nchini, ikiwemo kuongeza rasilimali fedha kwa ajili ya upangaji wa matumizi ya ardhi.

 

Amesema Serikali kwa kipindi cha miaka minne iliyopita, fedha zilizotengwa zilifanikisha Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji zaidi ya 4,000, hatua ambayo ni kubwa na inaonesha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha ardhi inapangwa na kutumika kwa tija.

 

Kwa mwaka wa fedha 2026/27, Tume imetengewa kiasi cha Sh. Bilioni 38 ambayo inatarajiwa kutekeleza uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi zaidi ya ya vijiji 1400. 

 

Kwa mwenendo huo wa bajeti hiyo, inatarajiwa vijiji vyote nchini kuwa vitaandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi ndani ya miaka minne ijayo.

 

Naibu Waziri pia amesisitiza umuhimu wa Tume kuendelea kushirikiana kwa karibu na Mamlaka za Upangaji na wananchi kwa ujumla, ili kuhakikisha wanafahamu maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli mbalimbali. Amesema ushirikishwaji huo utaongeza uwazi, uelewa na uwajibikaji katika matumizi ya ardhi, sambamba na kupunguza migogoro inayoweza kujitokeza kutokana na matumizi yanayokinzana.

 

Katika hatua nyingine, ameitaka Tume kuhakikisha kuwa vijiji vyote vinavyopitiwa na miradi ya kimkakati vinaingizwa katika programu za uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi, akieleza kuwa uzoefu unaonesha kuwa maeneo yanayopitiwa na miradi mikubwa ya kimkakati huwa na kasi kubwa ya ukuaji na hivyo yanahitaji maandalizi ya mapema ya mipango ya matumizi ya ardhi.