Habari
TNGC YAKAMILISHA MAANDALIZI YA UDAHILI WANAFUNZI KATIKA KOZI YA UPIMAJI ARDHI KWA KUTUMIA NDEGE ISIYO NA RUBANI NA SATELITE
- 24 Jun, 2026
Kituo cha Taifa cha Ubunifu na Mafunzo ya Taarifa za Kijografia (TNGC) kimekamilisha maandalizi ya kuanza kudahili wanafunzi wa ngazi za Cheti na Astashahada katika kozi ya upimaji ardhi kwa kutumia ndege isiyo na rubani pamoja na satellite (Drone Mapping and Satellite Surveying) kwa mwaka wa masomo 2026/27.
Hatua hiyo inafuatia watumishi wa kituo hicho cha TNGC kilicho ndani ya Chuo Kikuu Cha Dodoma (UDOM) kupatiwa mafunzo ya matumizi ya mfumo wa udahili wa NACTVET unaojulikana kama Central Admission System (CAS).
Akitoa mafunzo hayo Juni 22, 2026 jijini Dodoma mtaalamu kutoka Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET), Bi. Aines Chasubutu, alisema mfumo huo una lengo la kuhakikisha udahili wa wanafunzi unafanyika kwa kuzingatia viwango vya kitaifa, huku ukirahisisha usajili, uthibitishaji wa sifa za waombaji na usimamizi wa taarifa za kitaaluma.
Bi. Chasubutu alieleza kuwa NACTVET ina jukumu la kuhakikisha vyuo vinatoa mafunzo yenye ubora unaokidhi mahitaji ya soko la ajira na kwamba taasisi zote zinapaswa kuzingatia taratibu, kanuni na vigezo vilivyowekwa katika udahili na utoaji wa mafunzo ili kuzalisha wahitimu wenye ushindani.
Mafunzo hayo yalilenga kuwajengea uwezo watumishi wa kituo Cha TNGC katika matumizi ya mfumo wa CAS pamoja na kuwaandaa kusimamia kwa ufanisi shughuli za kitaaluma, zikiwemo udahili wa wanafunzi, usimamizi wa mitihani na utekelezaji wa viwango vya ubora vinavyotakiwa katika taasisi za elimu ya ufundi na elimu ya kati.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mkuu wa TNGC, Dkt. Aidan Kawinga, aliishukuru NACTVET kwa mafunzo hayo, akisema yamekuja wakati muafaka wakati kituo hicho kikijiandaa kuanza rasmi kutoa mafunzo.
"Tulikuwa na changamoto mbalimbali hususan katika masuala ya udahili, utawala wa taaluma na uhakiki wa ubora wa elimu. Tunawashukuru NACTVET kwa kutupatia mafunzo haya ambayo yametujengea uwezo wa kutumia kikamilifu mfumo wa CAS. Sasa tupo tayari kupokea na kufundisha wanafunzi," alisema Dkt. Kawinga.
Aliongeza kuwa hatua zinazofuata ni kukamilisha uingizaji wa mitaala katika mfumo wa CAS pamoja na kuendelea kuwajengea uwezo watumishi wanaosimamia utawala wa taaluma na mitihani ili kuhakikisha huduma zinatolewa kwa ufanisi.
TNGC, ambayo ipo chini ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), inatarajia kuanza kutoa mafunzo ya Drone Mapping and Satellite Surveying katika ngazi za Cheti na Astashahada, hatua inayotarajiwa kuongeza wataalamu wenye ujuzi wa teknolojia za kisasa katika sekta ya ardhi, upimaji na uchambuzi wa taarifa za kijiografia nchini.