Habari

TENGENEZENI WATAALAMU WENYE TIJA KUSAIDIA MPANGO WA MATUMIZI BORA YA ARDHI – MHE. MMUYA

  • 12 Jan, 2026
TENGENEZENI WATAALAMU WENYE TIJA KUSAIDIA MPANGO WA MATUMIZI BORA YA ARDHI – MHE. MMUYA

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Kaspar Mmuya amekitaka Chuo cha Ardhi Tabora (ARITA) kuandaa wataalamu wenye tija kwa kutafsiri nadharia wanazojifunza chuoni katika vitendo ili kusaidia utekelezaji wa mpango wa matumizi bora ya ardhi nchini.

Mhe. Mmuya ameyasema hayo tarehe 10 Januari, 2026 wakati akizungumza na wanafunzi wa Chuo hicho katika ziara yake ya siku mbili mkoani Tabora iliyolenga kufahamu maendeleo ya chuo hicho.

“Kwa nini sisi tusiwe na wataalamu katika eneo tunalojivunia? Tupike watoto wetu ili watoke wakiwa ni nguvu kazi yenye tija na ujuzi unaohitajika katika sekta ya ardhi,” amesema Mhe. Mmuya.

Ameeleza kuwa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Leonard Akwilapo ni kuhakikisha kila kipande cha ardhi nchini kinapimwa, kinapangwa na kumilikishwa.

Kutokana na hilo, amesema Chuo cha Ardhi Tabora kinapaswa kuandaa mpango mkakati wa kuwawezesha wanafunzi kushiriki moja kwa moja katika shughuli za upimaji, upangaji na umilikishaji wa ardhi ili kuwajengea ujuzi wa vitendo wakiwa bado chuoni.

“Tufanye shughuli zitakazoleta tija inayoonekana ili wanafunzi hawa washiriki na waone wanachojifunza wakiwa chuoni,” ameongeza.

Amebainisha kuwa utekelezaji wa maelekezo hayo utasaidia pia kugusa changamoto ya ajira kwa kuwa wahitimu watakuwa tayari kwa soko la ajira mara baada ya kuhitimu masomo yao.

Kwa upande wake, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Tabora Mhe. Gulam Dewji amewaasa wanafunzi wa Chuo hicho kuzingatia kikamilifu ujuzi wanaopatiwa chuoni ili wawe wataalamu bora wanaozingatia uadilifu katika utendaji wao wa kazi.

“Zingatieni ujuzi mnaopatiwa hapa chuoni ili mje kuwa watumishi bora wanaozingatia uadilifu katika taaluma zenu,” amesema Mhe. Dewji.

Naye rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo cha Ardhi Tabora (ARITA) Bw. Jackson Mchele amemuomba Naibu Waziri kukijumuisha Chuo hicho katika mpango wa matumizi bora ya ardhi wenye thamani ya shilingi bilioni 83.4 wa kipindi cha miaka 15 kuanzia mwaka 2023 hadi 2038 ili chuo kiweze kunufaika na huduma mbalimbali ikiwemo uboreshaji wa madarasa na viwanja vya michezo.

Amesema wanafunzi wa chuo hicho wana imani na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na hawapo tayari kuvuruga amani ya nchi.

“Sisi kama vijana hatupo tayari kuharibu amani ya nchi yetu,” amesema Bw. Mchele.

Naibu Waziri Mhe. Kaspar Mmuya amehitimisha rasmi ziara yake ya siku mbili mkoani Tabora ambapo alikagua ujenzi wa jengo la Tabora Biashara Complex linalojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa, alitembelea Chuo cha Ardhi Tabora pamoja na kufanya kikao na watumishi wa sekta ya ardhi mkoani humo.