Habari
TANZANIA YAWEKA MIKAKATI YA KUONGEZA UPATIKANAJI WA MAKAZI BORA NA YENYE NAFUU
- 16 Nov, 2026
Serikali ya Tanzania imeendelea kuweka mikakati ya kuongeza upatikanaji wa makazi bora, salama na yenye gharama nafuu kupitia Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, inayolenga upatikanaji wa nyumba milioni moja nchini.
Hayo yamesemwa leo Novemba 11, 2026, na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Kaspar Mmuya, akizungumza katika Mkutano wa 42 wa Mwaka na Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Umoja wa Afrika wa Ufadhili wa Nyumba (African Union for Housing Finance – AUHF), uliofanyika mjini Lusaka, Zambia.
Mkutano huo unalenga kuendeleza upatikanaji wa fedha za nyumba nafuu barani Afrika kupitia ubunifu, teknolojia na ushirikiano wa wadau wa sekta ya makazi.
Mhe. Mmuya amesema Tanzania inakabiliwa na upungufu wa nyumba unaokadiriwa kufikia vitengo milioni tatu, huku mahitaji mapya yakiongezeka kwa takribani vitengo 391,000 kila mwaka.
Katika kukabiliana na hali hiyo, Serikali kupitia Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) inalenga kujenga nyumba 5,000 ifikapo mwaka 2030, huku vitengo 560 vikiwa vimekamilika Kawe na vingine 660 vikiendelea kujengwa Njedengwa, Medeli na Iyumbu.
Aidha, amesema juhudi hizo zinaimarishwa na mchango wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) katika ujenzi na upatikanaji wa nyumba, pamoja na TMRC ambayo hadi Mei 2026 iliwezesha upatikanaji wa Shilingi bilioni 720.81 kupitia taasisi 29 za kifedha, zilizowanufaisha wananchi 5,802.
Ameongeza kuwa matumizi ya mifumo ya kidijitali ya e-Ardhi na huduma za Kliniki za Ardhi yanachangia kuimarisha usalama wa milki za ardhi, hatua muhimu katika kukuza uwekezaji na upatikanaji wa makazi bora na endelevu.
AUHF ilianzishwa mwaka 1984 kwa lengo la kuunganisha taasisi za fedha na wadau wa sekta ya nyumba ili kuongeza upatikanaji wa fedha na makazi nafuu barani Afrika, ambapo nchini Tanzania, juhudi hizo zinaendana na hatua zinazotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuelekea Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 kwa kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata makazi bora, salama na yenye gharama nafuu.