Habari
TANZANIA YATAJA VIPAUMBELE VITATU KUTEKELEZA AJENDA MPYA YA MIJI HADI 2036
- 20 Jul, 2026
Serikali ya Tanzania imetaja vipaumbele vitatu vitakavyoiongoza kuharakisha utekelezaji wa Ajenda Mpya ya Miji (New Urban Agenda) hadi mwaka 2036, vikilenga kuongeza upatikanaji wa makazi bora na nafuu, kuboresha huduma za msingi pamoja na kuimarisha ushiriki wa serikali za mitaa na wananchi katika maendeleo ya miji.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhandisi Anthony Sanga, wakati akiwasilisha taarifa ya Tanzania katika Mkutano wa Ngazi ya Juu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Makazi (UN-Habitat) kuhusu mapitio ya utekelezaji wa Ajenda Mpya ya Miji kwa kipindi cha miaka 10, mwishoni mwa wiki katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, New York.
Akizungumza katika jopo la majadiliano lenye kaulimbiu "Delivering for People: Scaling Adequate Housing, Land, Basic Services and Inclusion," Mhandisi Sanga alisema Tanzania imeendelea kupanua upatikanaji wa makazi bora na ya gharama nafuu kupitia kuimarisha usalama wa umiliki wa ardhi, kurasimisha makazi yasiyopangwa na kuongeza maeneo yaliyopangwa kwa ajili ya maendeleo ya makazi.
‘’Serikali ya Tanzania imefanya maboresho ya sera na mifumo ya kisheria ili kuwezesha uwekezaji katika sekta ya makazi, huku wananchi wakiruhusiwa kujenga nyumba zao baada ya kupata kibali cha mipango miji na ujenzi’’. Alisema Mhandisi Sanga
Aidha, alibainisha kuwa Serikali imeendelea kushirikiana na taasisi zake ikiwemo Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) na Watumishi Housing Investments (WHI) kujenga nyumba za aina mbalimbali kwa ajili ya kuuza na kupangisha, huku akisisitiza kuwa suluhisho la changamoto za makazi halitegemei ujenzi pekee bali pia linahitaji haki salama za umiliki wa ardhi, mifumo bora ya usimamizi wa ardhi, upatikanaji wa fedha za makazi na ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na jamii.