Habari

TANZANIA YAUNGA MKONO JUKWAA LA KIMATAIFA LA KUBADILISHANA TAARIFA NA UTAALAMU WA SEKTA YA MAKAZI

  • 27 Nov, 2026
TANZANIA YAUNGA MKONO JUKWAA LA KIMATAIFA LA KUBADILISHANA TAARIFA NA UTAALAMU WA SEKTA YA MAKAZI

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepongeza hatua zinazopigwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Makazi (UN-Habitat) katika kuanzisha Jukwaa la Maarifa kuhusu Makazi (Housing Knowledge Platform), ikieleza kuwa jukwaa hilo litakuwa nyenzo muhimu katika kuimarisha ubadilishanaji wa maarifa, matumizi ya takwimu na ushahidi katika uandaaji wa sera, pamoja na ushirikiano wa kimataifa katika kuhakikisha wananchi wanapata makazi bora na yanayomudu gharama.

 

Katika taarifa yake iliyotolewa Novemba 27, 2026, Tanzania imesisitiza umuhimu wa kuhakikisha nchi wanachama zinashirikishwa kikamilifu na kuwa na umiliki katika uanzishaji, usimamizi na uboreshaji endelevu wa jukwaa hilo, hususan nchi zinazoendelea ili kuhakikisha mahitaji na vipaumbele vyao vinazingatiwa.

 

Aidha, Tanzania imeeleza umuhimu wa jukwaa hilo kuzingatia changamoto mbalimbali za sekta ya makazi na mazingira ya kipekee ya kila nchi, kwa kuipa kipaumbele masuala ya makazi yasiyopangwa, upatikanaji wa nyumba za gharama nafuu, upatikanaji wa ardhi, mifumo ya ufadhili wa makazi, uendelezaji wa makazi kwa awamu pamoja na ujenzi wa makazi yanayokabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

 

Tanzania pia imesisitiza umuhimu wa kuimarisha ukusanyaji, uwekaji katika mifumo inayofanana na usasishaji wa mara kwa mara wa takwimu za sekta ya makazi ili kuwezesha maamuzi yanayotegemea taarifa sahihi na kurahisisha ufuatiliaji wa hatua zinazopigwa katika kuhakikisha kila mtu anapata makazi bora.

 

Aidha Tanzania imeishauri UN-Habitat kuhakikisha jukwaa hilo linaendana na mifumo ya kitaifa na kikanda ya ukusanyaji na usimamizi wa taarifa iliyopo, kuwezesha mifumo hiyo kuwasiliana na kubadilishana taarifa, pamoja na kuepuka kurudia mipango na juhudi ambazo tayari zinaendelea kutekelezwa.

 

Katika kuhakikisha jukwaa hilo linakuwa endelevu, Tanzania imeeleza umuhimu wa kuwepo kwa huduma za lugha mbalimbali, kujenga uwezo wa kitaalamu kwa nchi wanachama na kuhakikisha upatikanaji wa   rasilimali fedha za kutosha ili kuhakikisha uendelevu wake kwa muda mrefu.

 

Aidha, nchi imependekeza jukwaa hilo lisitumike kama hifadhi ya taarifa pekee, bali liwe nyenzo ya vitendo katika kubadilishana suluhisho bunifu, kuwezesha ushirikiano wa kitaalamu na kuhamasisha uwekezaji katika ujenzi wa nyumba za gharama nafuu na makazi bora.

 

Tanzania imethibitisha utayari wake wa kuchangia uzoefu wa kitaifa, mbinu bora na mafunzo iliyoyapata katika utekelezaji wa programu mbalimbali za sekta ya makazi, hususan urasimishaji wa makazi yasiyo rasmi, uendelezaji wa ardhi yenye huduma za kijamii na kiuchumi, upatikanaji wa nyumba za gharama nafuu na maendeleo endelevu ya makazi.

 

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesisitiza dhamira yake ya kuendelea kushirikiana na jumuiya ya kimataifa katika juhudi za kuhakikisha kila mtu anapata makazi bora, salama na yenye gharama nafuu.