Habari

TANZANIA NA MSUMBIJI ZAJADILI UIMARISHAJI MPAKA WA KIMATAIFA

  • 15 May, 2026
TANZANIA NA MSUMBIJI ZAJADILI UIMARISHAJI MPAKA WA KIMATAIFA

Serikali za Tanzania na Msumbiji ziko katika majadiliano ya uhakiki wa uimarishaji mpaka wa kimataifa kati ya nchi hizo mbili katika eneo la mto Ruvuma pamoja na kilomita 51 za nchi kavu.

 

Kikao cha Kamati ya Pamoja cha Wataalamu wa Tanzania na Msumbiji (JTC) kuhusu uhakiki wa mpaka huo kimeanza leo tarehe 12 Mei 2026 na kinatarajiwa kukamilika 15 Mei 2026.

 

Akifungua kikao hicho, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bi Lucy Kabyemera, alisema Tanzania na Msumbiji zina historia ya uhusiano wa kindugu unaowaunganisha wananchi wanaoishi mpakani.

 

Alisema, ushirikiano huo ni muhimu katika kuhakikisha amani, utulivu na ulinzi wa mipaka unaendelea kuimarika kati ya nchi hizo mbili.

 

Zoezi la uimarishaji mipaka ya kimataifa ni utekelezaji wa makubaliano ya umoja wa Afrika kuwa ifikapo mwaka 2027 mipaka baina ya nchi za Afrika iwe imeimarishwa.

 

Tanzania imepakana na nchi 10 ambazo ni Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, DRC, Zambia, Malawi, Msumbiji, Comoro na Shelisheli huku mipaka baina ya nchi hizo ikiwa imegawanyika katika sehemu mbili za nchi kavu na majini.