Habari

TABORA YATATUA MGOGORO WA ARDHI ILIYOMILIKISHWA TOKA  MIAKA YA 1969

  • 02 Oct, 2026
TABORA YATATUA MGOGORO WA ARDHI ILIYOMILIKISHWA TOKA  MIAKA YA 1969

Kliniki ya Ardhi Kidijiti inayoendelea mkoani Tabora imefanikisha utatuzi wa mgogoro wa ardhi uliodumu kwa muda mrefu kati ya familia ya Bi. Osiana Ahadi Shauri na familia ya Saidi Senyange, kuhusu maeneo ambayo familia hizo zimekuwa na nyaraka za umiliki tangu miaka ya 1982 na 1989.

 

Akizungumza wakati wa utatuzi wa suala hilo, Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Tabora, Bw. Tumaini Gwakisa, amesema kwa mujibu wa Mchoro wa Mipango Miji wa mwaka 1969, maendelezo yaliyofanywa na familia hizo yalitambuliwa, huku upimaji uliofanyika mwaka 2012 ukizingatia maendelezo yaliyokuwa yametambuliwa katika mchoro huo.

 

Amesema familia hizo zinamiliki maeneo mawili tofauti yaliyopo ndani ya kitalu kimoja, ambayo yametambuliwa kwa mujibu wa Ramani ya Upimaji na Michoro ya Mipango Miji. Aidha, ameeleza kuwa mabadiliko ya namba za viwanja au mashamba hayafuti wala kuondoa haki ya umiliki iliyokuwepo awali, endapo umiliki huo unatambulika katika kumbukumbu rasmi za ardhi.

 

Bw. Gwakisa amesema kuwa kwa kuzingatia taarifa na kumbukumbu za ardhi zilizopo, maeneo hayo hayana mgogoro wa msingi wa umiliki, kwa kuwa viwanja vyote saba vimepimwa na vipo tayari kwa hatua za umilikishaji. 

 

Aidha,amewataka wananchi husika kukamilisha malipo ya gharama za umilikishaji ili kuwezesha kuandaliwa na kutolewa kwa Hati za Miliki za maeneo yao.

 

Kliniki ya Ardhi Kidijiti imeendelea kuwa jukwaa muhimu la kuwafikishia wananchi huduma, elimu na ufafanuzi kuhusu masuala ya ardhi, ikiwemo utatuzi wa migogoro kwa kutumia taarifa sahihi za mipango miji, upimaji na kumbukumbu za ardhi. Hatua hiyo inachangia kuimarisha usalama wa milki na kupunguza migogoro ya ardhi nchini.