Habari
SERIKALI YAWEKA MSINGI IMARA WA USIMAMIZI WA ARDHI NA USANIFU WA MIJI
- 13 Feb, 2026
Wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii wamepata semina juu ya utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Ardhi ya Mwaka 1995 (Toleo la mwaka 2023) pamoja na vigezo vya usanifu wa miji nchini.
Wakiwasilisha kwenye kamati hiyo, Kamishna wa Ardhi Bw. Nathaniel Mathew na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Makazi Bw. Deogratias Kalimenze, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo, wameeleza kuwa lengo la Wizara na Wabunge ni kupata uelewa wa pamoja katika kuimarisha usimamizi wa ardhi, kupunguza migogoro na kuhakikisha ukuaji wa miji unaendana na mahitaji ya sasa na ya baadaye.
Mawasilisho hayo yameonesha mwelekeo wa Serikali wa kuoanisha Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995 (Toleo la 2023) na vigezo vinavyotumika kwenye upangaji miji, ili kukidhi mahitaji ya watu wanaoongezeka kwa kasi.
Kupitia maboresho hayo, Serikali inalenga kuwa na miji yenye miundombinu imara, huduma bora za jamii, ukuaji wa uchumi na ulinzi wa mazingira, huku ikiweka misingi madhubuti ya usimamizi endelevu wa ardhi nchini.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Mary Masanja akiongea kwa niaba ya kamati alisema ameridhishwa na jitihada hizo za wizara na kuahidi kuwapa ushirikiano ikiwepo wao kuwa mabalozi wa zuri katika kuhakikishausimamizi wa ardhi unaimarishwa.