Habari
SERIKALI YAWATOA HOFU WANANCHI UWEKEZAJI KIWANDA CHA SUKARI KOROGWE
- 18 Mar, 2026
Mkuu wa wilaya ya Korogwe mkoani Tanga Bwana William Simon, amewatoa hofu wananchi wa wilaya yake kuhusiana na uwekezaji mkubwa wa kiwanda cha sukari na kilimo cha miwa unaoenda kufanyika wilayani humo.
Bwana Simon ametoa kauli hiyo leo tarehe 17 Machi 2026 katika ukumbi wa halmashauri ya Korogwe DC mkoani Tanga wakati wa kikao maalum cha kuratibu na kuandaa utekelezaji wa mradi wa uwekezaji wa kilimo cha miwa na ujenzi wa kiwanda cha sukari unaotarajiwa kuanza hivi karibuni wilayani humo.
Kikao hicho kimehusisha wataalam kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wawekezaji wa Mradi huo pamoja na viongozi wa wilaya ya Korogwe.
Amesema, mradi huo unaenda kuwa chachu ya maendeleo katika wilaya hiyo huku akiahidi kuwa haki za wananchi zitalindwa kikamilifu katika kila hatua ya utekelezaji wake.
"Mradi huu unaenda kuwa chachu ya kuleta maendeleo katika wilaya hii ya korogwe na niwaahidi haki za wananchi zitalindwa kikamilifu katika kila hatua ya utekelezaji wake". Amesema
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe DC Bw. Goodluck Abinala ameeleza kuwa, mradi huo unahusisha ujenzi wa kiwanda katika Kata ya Makuyuni na unatarajia kutoa ajira kwa zaidi ya watu elfu kumi, huku shughuli zote za mradi zikifanyika ndani ya wilaya na hivyo kufungua fursa pana za kiuchumi kwa wananchi.
Akizungumza katika kikao hicho,kwa niaba ya Mthamini Mkuu, Bw. Rashid Mageta amesema, zoezi la uthamini wa fidia kwa eneo linaloenda kupisha mradi litafanyika kwa kuzingatia sheria na inalenga kulinda haki za wananchi wote watakaoguswa na mradi huo.
Amefafanua kuwa, fidia itahusisha Ardhi, mazao, makaburi na mali nyingine zote, huku akisisitiza kuwa hatua ya sasa ni utoaji elimu kabla ya kuanza kazi ya uwandani kukusanya taarifa na kuhakiki mipaka pamoja na mali za wananchi ili kuhakikisha kila mwenye stahiki analipwa kwa haki.
Mwekezaji, Eng Nixon Mrinji ameeleza kuwa, mradi wa uwekezaji kiwanda cha sukari na kilimo cha miwa ni kuunga mkono juhudi za serikali katika kukuza uwekezaji wa kilimo cha miwa mkoani Tanga.
Eneo linalotegemewa kutwaliwa ni hekta 83,012 ingawa utekelezaji utaanzia na hekta 47,663 na baadae maeneo mengine huku taratibu za uthamini zikiendelea katika kata za Mkomanzi, Mkalamo, Mazinde na Mkumbara, sambamba na utoaji wa ajira, mafunzo kazini, huduma za kijamii na kuongeza usalama wa chakula pamoja na mapato ya serikali.