Habari

SERIKALI YATOA ONYO KALI KWA WAVAMIZI WA MAENEO YA WAZI

  • 12 May, 2026
SERIKALI YATOA ONYO KALI KWA WAVAMIZI WA MAENEO YA WAZI

Serikali imetoa onyo kali kwa watu wote wanaovamia na kujenga katika maeneo ya wazi bila kufuata taratibu za kisheria, ikisisitiza kuwa itachukua hatua za kubomoa majengo hayo bila kujali gharama kubwa zilizotumika katika ujenzi.

 

Akizungumza Bungeni jijini Dodoma Mei 11, 2026, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Kaspar Mmuya, amesema serikali imeweka misingi imara ya kisheria na sera ili kusimamia sekta ya ardhi kwa ufanisi, ikiwemo Sera ya Maendeleo ya Makazi ya mwaka 2000 na maboresho ya hivi karibuni ya Sheria ya Mipango Miji.

 

Mhe. Mmuya amebainisha kuwa serikali imefanya kazi kubwa ya kuweka misingi imara ya kisera na sheria ili kuhakikisha sekta hiyo inasimamiwa kwa weledi. 

 

Ameitaja Sera ya Maendeleo ya Makazi ya mwaka 2000, Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995 (Toleo la mwaka 2023), pamoja na Sheria ya Mipango Miji Sura ya 355 kuwa ndizo nyenzo kuu zinazotumika sasa kupanga, kumilikisha, na kusimamia matumizi ya ardhi nchini kote.

 

Naibu Waziri huyo alifafanua kuwa uwepo wa kanuni za sheria za Sheria ya Mipangomiji Sura 355 za mwaka 2018 na maboresho yake ya mwaka 2023 zimesaidia kuimarisha usimamizi wa ardhi kwa ajili ya kulinda maslahi ya umma na kuhakikisha kuwa kila kipande cha ardhi kinatumika kulingana na mpango uliowekwa na mamlaka husika bila kuingiliwa na watu binafsi.

 

Aidha, Mhe. Mmuya alitoa tahadhari kwa wale wote ambao wamekuwa na tabia ya kukiuka maelekezo ya serikali kwa kujenga katika maeneo yasiyoruhusiwa akisisitiza kuwa maelekezo ya Waziri wa Ardhi yako wazi, na operesheni za kubomoa zitafanyika kuanzia hatua ya maandalizi ya ujenzi, hatua ya msingi, hadi majengo yaliyokamilika ikiwa yatabainika kukiuka mipango miji.