Habari
SERIKALI YATENGA BILIONI 38 KUPIMA VIJIJI VYOTE TANZANIA, YAAGIZA KLINIKI ZA ARDHI KILA KATA
- 02 Jul, 2026
Serikali imetangaza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameridhia utoaji wa kiasi cha shilingi bilioni 38 kwa ajili ya kufanikisha mpango wa kupima vijiji vyote nchini ili kumaliza migogoro ya ardhi.
Hayo yameelezwa leo Julai 1, 2026 katika viwanja vya Sokoni Mugumu Wilaya ya Serengeti mkoani Mara na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Kaspar Mmuya alipokuwa akizungumza mbele ya Waziri Mkuu, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, ambaye yuko katika ziara ya kikazi ya siku tano mkoani humo.
Katika hatua ya haraka ya kusogeza huduma kwa wananchi, Mhe. Mmuya amemuagiza Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Mara pamoja na timu yake, kuhakikisha wanaratibu na kuanzisha kliniki za ardhi katika kila kata.
"Hakikisheni mnaratibu uwepo wa kliniki za ardhi katika kila kata ili muwasikilize wananchi hawa na msione kila changamoto mpewazo ni ya mazoea. Hapana, amekuja kwako kwa sababu ana jambo la kusikilizwa na litatuliwe," alisema Naibu Waziri Mmuya.
Mhe. Mmuya alieleza kuwa wizara ya Ardhi iliwasilisha mpango na maombi ya fedha bungeni kufuatia maelekezo ya awali ya Waziri Mkuu, na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan akaidhinisha shilingi bilioni 38 kwa ajili ya kupima jumla ya vijiji 12,333 vya Tanzania.
"Mpaka hivi ninavyoongea, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kipindi chake kifupi tu ameweza kupima vijiji 4,873. Na ametupatia maelekezo kuwa ndani ya kipindi chake, vijiji vyote vilivyobakia tuvipime." Aliongeza Naibu Waziri Kaspar Mmuya
Katika hatua nyingine Mhe. Mmuya amesema Wizara ya Ardhi itashirikiana bega kwa bega na Ofisi ya Rais - TAMISEMI ili kuhakikisha maagizo hayo yanatekelezwa kikamilifu katika vijiji vyote vilivyosalia nchini.
Aidha, Mhe. Mmuya alieleza kuwa Wilaya ya Serengeti ina kata 30 na vijiji 78. Ameuhakikishia uongozi wa wilaya hiyo kuwa vijiji vyote 78 vimeshaingizwa kwenye mpango wa upimaji ndani ya kipindi cha miaka mitano ya Rais Samia Suluhu Hassan.
"Kupima vijiji hivi ndiyo dawa kubwa ya kutatua changamoto ya mipaka kati ya kijiji na kijiji. Lakini ni dawa kubwa ya kutatua changamoto ya kugombania matumizi ya ardhi ya mtu mmoja mmoja, taasisi na taasisi, au serikali na wananchi," alisema Naibu Waziri Kaspar Mmuya.