Habari

SERIKALI YASISITIZA ULIPAJI KODI YA ARDHI KWA WAKATI

  • 23 Apr, 2026
SERIKALI YASISITIZA ULIPAJI KODI YA ARDHI KWA WAKATI

Serikali imewataka wamiliki wote wa ardhi nchini wakiwemo watu binafsi na taasisi zinazomiliki ardhi kuhakikisha zinalipa kodi ya pango la ardhi kwa wakati, ili kuepusha usumbufu utakaotokana na hatua zitakazochukuliwa kwa wale watakaoshindwa kutekeleza wajibu huo.

 

Akizungumza jijini Dodoma Aprili 22, 2026 wakati wa kikaona  kutathmini  utekelezaji wa mikakati 12 ya kudai kodi ya pango la ardhi na waratibu wa kodi mkoa wa Dodoma na wilaya zake,Kamishna Msaidizi wa Ardhi anayeshughulikia Uwekezaji na Mapato kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bw. Leonard Melchior Msafiri, amesema utekelezaji wa agizo hilo unatokana na maelekezo ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo.

 

Amesisitiza kuwa ulipaji wa kodi ya pango la ardhi si hiari bali ni wajibu wa kisheria kwa kila mmiliki wa ardhi, akibainisha kuwa Serikali haitavumilia uzembe au ukaidi katika suala hilo.

 

Kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi Sura ya 113, hasa vifungu vya 48(1), 50, 51 na 52, mmiliki yeyote atakayeshindwa kulipa kodi hiyo kwa wakati atachukuliwa hatua za kisheria, ikiwemo kufikishwa mahakamani na kufutiwa umiliki wa ardhi husika.

 

Bw. Msafiri ameeleza kuwa ucheleweshaji wa malipo husababisha kuongezeka kwa malimbikizo ya madeni pamoja na riba, hali inayoweza kuwa mzigo mkubwa kwa wadaiwa na kuathiri mipango yao ya kifedha.

 

Amesema waratibu wa ukusanyaji kodi ya pango la ardhi kutoka mikoa mbalimbali wamekutana Dodoma kwa lengo la kufanya tathmini ya utendaji na kuweka mikakati madhubuti ya kufikia lengo la ukusanyaji wa shilingi bilioni 290 kwa mwaka wa fedha 2025/2026.

 

Bw.Msafiri amesema miongoni mwa mikakati iliyowekwa ni pamoja na kuwafikia wadaiwa wote wa kodi hiyo nchini, bila kujali kama ni wamiliki binafsi au taasisi za umma, ili kuhakikisha kila mmoja anatimiza wajibu wake.

 

“Mikoa yote imeelekezwa kuweka mikakati thabiti ya kufikia malengo ya ukusanyaji wa mapato ya kodi ya pango la ardhi,” amesema 

 

Aidha, ofisi zote za ardhi nchini zimeelekezwa kusimamia kikamilifu zoezi la ukusanyaji wa kodi hiyo, huku hatua kali zikitarajiwa kuchukuliwa kwa watakaokiuka sheria, ikiwemo kutozwa faini na hatua nyingine za kisheria.