Habari
SERIKALI YASISITIZA ULINZI NA USIMAMIZI WA MAENEO YA WAZI NCHINI
- 16 Apr, 2026
Serikali imezitaka Mamlaka za upangaji nchini kuhakikisha maeneo ya wazi yanapangwa, yanalindwa na kuendelezwa kwa kuzingatia sheria, sera na kanuni zilizopo, ili kulinda maslahi ya umma na matumizi endelevu ya ardhi.
Hayo yameelezwa bungeni leo tarehe 15 Aprili 2026 na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Kaspar Mmuya wakati akijibu swali la Mbunge Husna Juma Sekiboko, aliyetaka kufahamu uwepo wa sheria zinazolinda maeneo ya wazi na viwanja vya michezo mijini na vijijini.
Amesema kuwa upangaji na usimamizi wa matumizi ya ardhi unaongozwa na sera, sheria na kanuni mbalimbali zinazolenga kulinda maeneo ya wazi, ikiwemo Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Makazi ya mwaka 2000 na Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995 (Toleo la 2023), pamoja na Sheria ya Mipango Miji, Sura ya 355 na kanuni zake.
Alifafanua kuwa sheria hizo zinatoa miongozo mahsusi ya kulinda maeneo ya wazi kwa matumizi ya umma, huku mamlaka husika zikipewa jukumu la kusimamia na kuhakikisha matumizi hayo hayakiuki mipaka iliyowekwa kisheria.
Aidha, alibainisha kuwa Serikali kupitia Mamlaka za Upangaji inaendelea kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha maeneo hayo hayavamwi wala kubadilishwa matumizi kiholela, ikiwa ni pamoja na kusimamia uuzaji, upangaji na uendelezaji wake kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa.
Maeneo ya wazi ni rasilimali muhimu katika kuhakikisha upangaji endelevu wa miji na vijiji. Yanachangia kuboresha afya ya jamii, kulinda mazingira na kuongeza ubora wa maisha ya wananchi kwa ujumla.