Habari

SERIKALI YASISITIZA MATUMIZI YA e-MREJESHO KUIMARISHA HUDUMA KWA WANANCHI

  • 15 May, 2026
SERIKALI YASISITIZA MATUMIZI YA e-MREJESHO KUIMARISHA HUDUMA KWA WANANCHI

Serikali imeendelea kusisitiza matumizi sahihi ya mfumo wa e-Mrejesho kama nyenzo muhimu ya kuimarisha uwajibikaji na kuongeza ubora wa huduma kwa wananchi katika taasisi za umma.

 

Hayo yamesemwa leo Mei 15, 2026 na Mkurugenzi wa Tathmini na Ufuatiliaji wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bi. Mariam Silimu, aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo wakati wa kufunga mafunzo ya matumizi ya mfumo wa e-Mrejesho yaliyowahusisha washiriki 28 kutoka Wizara pamoja na taasisi mbalimbali za sekta ya ardhi.

 

Bi. Silimu amesema Serikali inatarajia kuona watumishi wakitumia mfumo huo kwa ufanisi zaidi ili kuhakikisha maoni, ushauri na changamoto za wananchi zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati na kwa weledi unaostahili.

 

Aidha, amewataka washiriki kuwa mabalozi wazuri wa mabadiliko katika taasisi zao kwa kutumia maarifa waliyopata kuongeza tija na kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi.

 

Akizungumza kwa niaba ya washiriki wa mafunzo hayo, Bw. Cathlex Makawia ambaye ni Afisa Utumishi mkuu wa Chuo cha Ardhi Tabora ( ARITA ), ameishukuru Serikali pamoja na Wizara kwa kuwajengea uwezo, huku akiahidi kuyafanyia kazi mafunzo hayo kwa matokeo chanya kwa taasisi zao na Serikali kwa ujumla.

 

Washiriki waliopata mafunzo hayo walitoka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC), Bodi ya Wathamini (VRB), Bodi ya Mipango Miji (TPRB), Chuo cha Ardhi Morogoro (ARIMO) pamoja na Chuo cha Ardhi Tabora (ARITA).