Habari

SERIKALI YASISITIZA KUTUMIA MBINU ZA KISAYANSI KATIKA KUTAMBUA NA KULINDA MAENEO HATARISHI NA NYETI

  • 21 Apr, 2026
SERIKALI YASISITIZA KUTUMIA MBINU ZA KISAYANSI KATIKA KUTAMBUA NA KULINDA MAENEO HATARISHI NA NYETI

Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Makazi kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bw. Deogratius Kalimenze, amehitimisha mafunzo ya siku sita kwa wadau wa sekta ya ardhi kutoka taasisi mbalimbali za serikali kwa kusisitiza umuhimu wa kutumia mbinu za kisayansi katika kutambua na kulinda maeneo hatarishi na nyeti.

 

Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo tarehe 18/04/2026 mkoanin Arusha. Bw. Kalimenze alisema kuwa pamoja na kuwepo kwa Sheria Namba 4 ya Ardhi inayotaja maeneo hatarishi na nyeti yanayopaswa kulindwa, bado baadhi ya maeneo hayajatangazwa rasmi kupitia Gazeti la Serikali kutokana na ukosefu wa ushahidi wa kisayansi.

 

Alieleza kuwa jukumu kubwa la serikali ni kuhakikisha miji inakuwa salama, jumuishi, stahimilivu na endelevu, hali inayohitaji kuzingatia kwa kina masuala ya kimazingira katika mipango ya maendeleo.

 

Katika kuimarisha juhudi hizo, alisema wizara kwa kushirikiana na TAMISEMI pamoja na Benki ya Dunia imechukua hatua mbalimbali za kuhakikisha miji inapangwa na kuendelezwa kwa kuzingatia usalama na uendelevu.

 

“Dunia inakwenda kwa kasi kubwa ya teknolojia katika utendaji wa kazi za kila siku. Ukikaa mbali na teknolojia, huwezi kuendana na mabadiliko yanayoendelea,” alisema Bw. Kalimenze.

Aliongeza kuwa mafunzo hayo, yaliyojumuisha matumizi ya teknolojia na majadiliano ya kitaalamu, ni msingi muhimu wa kupata majibu ya kisayansi yatakayosaidia kutambua maeneo hatarishi na kulinda maeneo nyeti.

 

Aidha, aliwataka washiriki kuhakikisha wanatumia maarifa waliyopata kwa vitendo badala ya kuyaacha darasani, akisisitiza kuwa wizara itafuatilia utekelezaji wake.

 

“Sisi kama wizara tutahakikisha mnawasilisha shapefiles za maeneo mliyoyafanyia kazi. Hii itasaidia kuyatambua rasmi na kuyapanga kwa usahihi,” alisisitiza.

 

Alibainisha kuwa wizara pia inaandaa mwongozo maalum utakaowasaidia wataalamu hao kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi na kuhakikisha taarifa wanazowasilisha zinakidhi viwango vinavyohitajika.