Habari

SERIKALI YASISITIZA ELIMU MATUMIZI YA MFUMO WA e-ARDHI KWA WANANCHI

  • 22 Sep, 2026
SERIKALI YASISITIZA ELIMU MATUMIZI YA MFUMO WA e-ARDHI KWA WANANCHI

Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera, Bw. Isaya Tendega amesisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu mfumo wa e-Ardhi ili waweze kuuelewa na kuutumia ipasavyo wakati wa kupata huduma za ardhi zinazotolewa kwa njia ya kidijiti.

 

Aidha, amewataka wataalamu wa ardhi kuwa karibu na wananchi na kuwapatia elimu sambamba na kuwaongoza katika matumizi ya mfumo huo.

 

Akizungumza katika hafla ya kuhitimisha mafunzo ya mfumo huo kwa wataalamu wa ardhi mkoani Kagera, Bw. Tendega amesema ujio wa e-Ardhi umefika wakati muafaka kwa Mkoa huo, kwa kuwa utarahisisha umilikishaji wa vipande vya Ardhi na kusaidia kukabiliana na changamoto za ardhi. 

 

Kwa upande wao, wananchi waliopokea hati milki za ardhi kupitia mfumo wa e-Ardhi mkoani Kagera wameeleza furaha yao kuhusu matumizi ya mfumo huo huku wakiuelezea kuwa unawawezesha kupata huduma kwa njia ya mtandao bila ulazima wa uwepo wao katika kila hatua ya mchakato.

 

Kwa upande wake, Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Kagera, Bi. Florida Busheni, amesema Wizara ya Ardhi imefanya juhudi kubwa kuhakikisha wataalamu wanapata ujuzi wa kutumia mfumo huo mpya kupitia mafunzo, na kwamba Kagera sasa iko tayari kutoa huduma za ardhi kwa njia ya kidijitali.

 

Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) Wizara ya Ardhi, Bw Adeladus Muttayabalwa amewahakikishia wananchi kuwa wataalamu wamejengewa uwezo na miundombinu hivyo wanaweza kuendelea kutumia programu ya e-Ardhi kupata huduma za ardhi.

 

Mafunzo hayo yamehitimishwa leo Septemba 21, 2026, katika ukumbi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (ELCT) Bukoba baada ya kufanyika kwa siku nane kuanzia Septemba 14, 2026, huku jumla ya hati tano zikitolewa kupitia mfumo huo wa kidijiti, ikiwa ni miongoni mwa matokeo ya mafunzo yaliyofanyika kwa vitendo.