Habari
SERIKALI YAPENDEKEZA UJENZI WA GHOROFA ARDHI HAIONGEZEKI
- 15 Jun, 2026
Serikali ya Tanzania imetangaza mkakati mpya wa kudhibiti matumizi ya ardhi nchini kwa kuweka mkazo mkubwa katika ujenzi wa majengo ya ghorofa, huku ikibainisha kuwa mbinu za zamani za ujenzi uliotawanyika zinasababisha gharama kubwa zisizo na tija kwa taifa.
Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Kaspar Mmuya, wakati akizungumza kwenye Mkutano Mkuu wa 45 wa Benki ya Maendeleo ya Makazi Barani Afrika (ShafDB) uliyofanyika katika Hoteli ya Sofitel jijini Rabat, Morocco
Mhe. Mmuya amesema kuwa rasilimali ya ardhi haiongezeki, hivyo kuna haja ya kubadili namna ya ujenzi wa makazi kuelekea Dira ya Maendeleo ya mwaka 2050 yenye lengo la Kuboresha Maisha ya kila mtanzania katika sekta ya makazi.
"Ardhi haiongezeki. Kwa hiyo ujenzi ambao tunautegemea... ni lazima uwe ujenzi wa majengo ya ghorofa. Tukijenga majengo ya ghorofa, kwanza tutaisaidia serikali kufikisha huduma zote za kijamii kwa mara moja kwa watu wengi kwa eneo dogo," alisisitiza Naibu Waziri Mmuya.
Naibu Waziri Mmuya aliongeza kuwa ujenzi wa ghorofa utapunguza mzigo wa kifedha kwa serikali katika kufuatilia makazi yaliyotawanyika kwa ajili ya kupeleka miundombinu ya msingi kama barabara, nishati ya umeme, na mifumo ya maji safi.
Kama sehemu ya kuchochea mabadiliko hayo, Mhe. Mmuya amebainisha mpango wa serikali wa kuondoa kabisa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa ujenzi wa nyumba zote za gharama nafuu zisizozidi shilingi milioni 50 ili kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, pamoja na sekta binafsi.
"Uwekezaji katika nyumba zote zenye gharama isiyozidi milioni 50, huyo uwekezaji katika jengo hilo hatatozwa VAT. Hii ni incentive (kivutio) kubwa sana," alifafanua Naibu Waziri Mmuya.
Mhe. Mmuya amekiri kuwa serikali pekee haiwezi kufikia malengo hayo makubwa ya ustawi wa jamii bila kushirikiana kikamilifu na sekta binafsi ambapo amebainisha kuwa Tanzania imeridhia na kukubaliana kuwa sekta binafsi ndiyo nguzo kuu itakayosaidia kuingiza mitaji na fedha kutoka ndani na nje ya nchi ili kufanikisha azma hiyo.
"Bila kushirikiana na sekta binafsi ili kuwasaidia kama nchi kupata fedha ndani na nje ya nchi, hatuteweza kufikia lengo hili. Kwa hiyo sisi kama Watanzania tumekubali baada ya mkutano huu," alifafanua Naibu Waziri Kaspar Mmuya.
Mara baada ya kukamilika kwa mkutano huo wa kimataifa nchini Morocco, Naibu Waziri amesema serikali itajikita katika vipaumbele viwili vikuu ikiwemo kuwasilisha taarifa kamili ya makubaliano hayo kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na kushirikiana na Wizara ya Fedha ili kurahisisha mawasiliano na kukutana na wawekezaji wote wenye nia ya kuwekeza katika ujenzi wa makazi hayo mapya ya ghorofa.