Habari

SERIKALI YAONGEZA KASI UPIMAJI ARDHI MAHOMANYIKA NA IPALA, DODOMA

  • 10 Apr, 2026
SERIKALI YAONGEZA KASI UPIMAJI ARDHI MAHOMANYIKA NA IPALA, DODOMA

Serikali imeendelea kuchukua hatua madhubuti za kuboresha usimamizi wa ardhi kwa kuimarisha zoezi la upimaji wa viwanja katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Dodoma, ikiwemo Kata za Mahomanyika na Ipala.

 

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mpima kutoka Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Dodoma, Bw. Bariheza Titi, amesema kazi ya upimaji inayoendelea inalenga kutafsiri mpango mji uliopo kwenye ramani na kuutekeleza moja kwa moja ardhini.

 

Amesema zoezi hilo linahusisha uwekaji wa alama maalum zitakazorahisisha utambuzi wa mipaka ya viwanja na matumizi yake, hatua itakayosaidia kuondoa mkanganyiko wa umiliki wa ardhi katika maeneo hayo.

 

Katika mchakato huo, wataalamu wanatumia alama za upimaji zikiwemo Beacons na Pins ili kubaini mipaka sahihi ya viwanja vitakavyotumika kwa shughuli mbalimbali kama makazi, biashara pamoja na maeneo ya wazi (Open Space)

 

“Tunachukua ramani ya mipango miji ya eneo hili na kuitafsiri ardhini kwa kuweka alama zitakazosaidia kupima na kutambua viwanja kwa matumizi mbalimbali. Zoezi hili linafanyika kwa kuzingatia mpango wa kitaifa wa upimaji wa ardhi,” amesema Bw. Titi.

 

Ameongeza kuwa, uamuzi wa kuanza kwa upimaji katika maeneo hayo umetokana na ongezeko la mahitaji ya ardhi, hususan kwa wananchi na wawekezaji wanaotaka kuendeleza makazi na shughuli za kiuchumi, jambo linalochochea ukuaji wa haraka wa Jiji la Dodoma.

 

Hatua hiyo inatarajiwa kuongeza umiliki rasmi wa ardhi, kupunguza migogoro ya mipaka na matumizi ya ardhi, pamoja na kuweka mazingira rafiki kwa uwekezaji na maendeleo endelevu ya makazi kwa wananchi.