Habari

SERIKALI YAIPA SEKTA YA UJENZI JUKUMU LA KIMKAKATI

  • 24 Sep, 2026
SERIKALI YAIPA SEKTA YA UJENZI JUKUMU LA KIMKAKATI

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo, amesema sekta ya ujenzi na majengo ni miongoni mwa sekta za kimkakati zitakazochochea utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050 na kufanikisha azma ya kujenga uchumi wa taifa wenye thamani ya dola trilioni moja ifikapo mwaka 2050.

 

Dkt. Akwilapo amesema hayo Septemba 23, 2026, wakati akifungua rasmi Maonesho ya 27 ya Kimataifa ya Ujenzi na Majengo, BuildExpo Tanzania, jijini Dar es Salaam.

 

Amesema Tanzania imeanza rasmi safari ya utekelezaji wa Dira 2050, inayolenga kuijenga nchi kuwa taifa lenye ustawi, uchumi jumuishi na linalojitegemea, huku ikitoa msukumo katika maeneo ya ustawi wa wananchi, ukuaji wa uchumi wenye tija na jumuishi, maendeleo endelevu, miundombinu ya kisasa na kuboresha mazingira ya maisha.

 

Kwa mujibu wa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, utekelezaji wa malengo hayo unahitaji sekta ya ujenzi kutazamwa kwa mtazamo mpana zaidi, badala ya kuichukulia kama shughuli ya kujenga nyumba na majengo pekee.

 

Amesema sekta hiyo ina nafasi ya kimkakati katika kujenga mazingira yatakayowezesha ukuaji wa uchumi, upatikanaji wa makazi bora, ujenzi wa miundombinu na kuboresha huduma muhimu kwa wananchi.

 

"Sekta ya ujenzi na majengo haipaswi kuonekana tu kama sekta inayojenga nyumba na majengo, bali ni sekta ya kimkakati katika kufikia matarajio yetu ya maendeleo ya taifa," amesema Dkt. Akwilapo.

 

Aidha, amesema mageuzi mbalimbali yanaendelea kufanyika kwa lengo la kuboresha mazingira ya biashara nchini, huku ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi kupitia mfumo wa Public-Private Partnerships (PPPs) ukipewa nafasi muhimu.

 

Amesema mfumo huo ni miongoni mwa mikakati inayoweza kusaidia kukabiliana na mahitaji yanayoongezeka ya ujenzi na miundombinu.

 

Ameongeza kuwa, Serikali inaendelea kuhimiza ushirikiano huo kupitia mifumo ya kisheria iliyowekwa chini ya Sheria ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi Na. 19 ya mwaka 2010.

 

Hata hivyo, Dkt. Akwilapo amesema mjadala wa maendeleo ya sekta ya ujenzi haupaswi kujikita katika swali la kama Tanzania itajenga, bali unatakiwa kuelekezwa zaidi katika aina ya teknolojia zitakazotumika kujenga mazingira yanayokidhi mahitaji ya kizazi kijacho.

 

Amefafanua kuwa, Tanzania inahitaji makazi yaliyopangwa vizuri, jumuishi, yanayomudu gharama, yenye tija kiuchumi, yanayozingatia mazingira na yenye uwezo wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

 

Amesema matumizi ya teknolojia sahihi ni muhimu katika kuhakikisha ujenzi wa nyumba, majengo na miundombinu unaendana na mahitaji ya sasa na yajayo.

 

Kwa mtazamo huo, amesema BuildExpo inatoa nafasi kwa wadau kuonesha teknolojia, vifaa na mbinu mpya zinazoweza kutumika katika kuendeleza sekta ya ujenzi nchini.

 

Amevitaka vikundi na taasisi mbalimbali vinavyohusika na ujenzi kutumia maonesho hayo kutafuta wasambazaji, washirika, vifaa na teknolojia zinazoweza kukidhi mahitaji yao.

 

Amesema ushiriki wa wataalamu, wawekezaji, wazalishaji, wakandarasi na taasisi mbalimbali katika jukwaa hilo ni muhimu katika kujenga uelewa wa pamoja kuhusu mwelekeo wa sekta ya ujenzi na mahitaji ya Tanzania katika utekelezaji wa Dira 2050.