Habari
SERIKALI YAFUNGUKA UTATUZI WA MGOGORO WA PORI LA SWAGASWAGA CHEMBA, EKARI ZINGINE ZAMEGWA KWA WANANCHI
- 24 Jun, 2026
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Kaspar Mmuya, amefafanua hatua zilizochukuliwa na Serikali katika kutatua mgogoro wa ardhi unaohusisha Pori la Swagaswaga wilayani Chemba, ambapo kilomita za mraba 7.85 zimemegwa kutoka katika pori hilo na kutengwa kwa matumizi ya wananchi wa vitongoji vya Mnang'ali, Ilala A, Ilala B na Mnang'a katika Kijiji cha Handa.
Mhe. Mmuya ametoa ufafanuzi huo Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Chemba, Mhe. Kunti Majalla.
Aidha, ameahidi kuwa kuanzia Julai 1 mwaka huu, Wizara itapeleka wataalamu wa ardhi, akiwemo Mthamini na Afisa Mipango Miji, ili kushughulikia na kumaliza changamoto mbalimbali za ardhi zinazowakabili wananchi wa wilaya hiyo.
Ameongeza kuwa mawaziri wa sekta husika, akiwemo Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Waziri wa Maliasili na Utalii pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, wamefikia makubaliano ya kutembelea Jimbo la Chemba kwa pamoja ili kutangaza rasmi maamuzi hayo kwa wananchi.
Akizungumzia changamoto ya upungufu wa watendaji katika sekta ya ardhi, Mhe. Mmuya amesema kuwa Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora iliajiri watumishi wapya 400 wa sekta hiyo katika mwaka huu wa fedha ambapo kuanzia Julai 1, Katibu Mkuu wa Wizara atateua na kuwatuma Chemba Mthamini na Afisa Mipango Miji, huku jitihada zikiendelea za kuwapata wenyeviti wa Mabaraza ya Ardhi ili kuimarisha utoaji wa huduma.