Habari

SERIKALI YAFUNGUKA KUHUSU MGOGORO WA MIPAKA KITONGOJI CHA MPANYANI MASASI

  • 04 Nov, 2026
SERIKALI YAFUNGUKA KUHUSU MGOGORO WA MIPAKA KITONGOJI CHA MPANYANI MASASI

Serikali imesema Kitongoji cha Mpanyani, kilichopo Kata ya Nangoo, Wilaya ya Masasi, Mkoa wa Mtwara, kiko ndani ya Ardhi ya Kijiji cha Muongozo na kwamba mgogoro unaohusishwa na eneo hilo si wa mipaka, bali unatokana na mgongano wa kimila unaohusiana na ukusanyaji wa ushuru wa mazao, hususan katika msimu wa korosho.

 

Hayo yamesemwa leo, Novemba 3, 2026, na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Kaspar Mmuya, wakati akijibu Swali Na. 91 lililoulizwa na Mbunge wa Ndanda, Mhe. Faraji Buriani Nandala, katika Kikao cha Sita cha Mkutano wa Tano wa Bunge, jijini Dodoma.

 

Katika swali hilo, Mbunge huyo alitaka kujua hatua ambazo Serikali itachukua kutatua mgogoro wa mipaka katika Kitongoji cha Mpanyani, Kata ya Nangoo, ili kubainisha kama eneo hilo lipo Wilaya ya Masasi au Newala.

 

Mhe. Mmuya amesema wakazi wengi wa Kitongoji cha Mpanyani ni wakulima, huku baadhi yao wakitokea Wilaya ya Newala katika vijiji jirani vilivyopo Kata ya Mikumbi.

 

Ameeleza kuwa mwaka 2018, Wizara kupitia iliyokuwa Ofisi ya Ardhi Kanda ya Kusini, kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara pamoja na Halmashauri za Wilaya za Masasi na Newala, ilishughulikia mgogoro huo.

 

Amebainisha uchunguzi uliofanyika wakati huo ulibaini kuwa hakukuwa na changamoto ya mpaka kati ya maeneo hayo, bali kulikuwa na mgongano wa kimila uliotokana na ukusanyaji wa ushuru wa mazao, hasa katika kipindi cha msimu wa korosho.