Habari
SERIKALI YAFANUA GHARAMA ZA UPIMAJI WA ARDHI
- 31 Aug, 2026
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Kaspar Mmuya amesema gharama za kupanga na kupima kiwanja kimoja katika maeneo yaliyoendelezwa zimepunguzwa hadi Shilingi 130,000, hatua inayolenga kupunguza mzigo wa gharama kwa wananchi.
Mhe. Mmuya amesema hayo leo Agosti 31, 2026, bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Mafinga Mjini, Mheshimiwa Dickson Nathan Lutevele, aliyehoji kuhusu lini Serikali itaanzisha utaratibu wa kupima ardhi kwa gharama nafuu kwa wananchi wa Kata za Isalavanu, Bumilayinga, Rungemba na Saohill.
Akifafanua kuhusu gharama za upimaji, Mhe. Mmuya amesema kwa maeneo yaliyoendelezwa, gharama za upimaji hutozwa kwa kuzingatia Mwongozo wa Urasimishaji wa Mwaka 2021.
Amesema kupitia mwongozo huo, gharama ya kupanga na kupima kiwanja kimoja kwa sasa ni Shilingi 130,000, ikilinganishwa na gharama za awali ambazo zilikuwa kati ya Shilingi 250,000 hadi Shilingi 400,000.
“Gharama ya kupanga na kupima kiwanja kimoja hivi sasa ni Shilingi 130,000,” amesema Mhe. Mmuya.
Aidha, kuhusu upimaji wa kawaida ambao hauhusishi urasimishaji, Naibu Waziri amesema utaratibu huo unaongozwa na Mwongozo wa Ukadiriaji Bei za Viwanja wa Mwaka 2016.
Amesema katika utaratibu huo, gharama za upimaji hutegemea vigezo mbalimbali, ikiwemo umbali wa eneo linalopimwa, ukubwa wa eneo, umbali kutoka kwenye alama za msingi zilipo, idadi ya vifaa vitakavyotumika katika kazi hiyo pamoja na gharama za alama za mipaka (Beacons).
Mhe. Mmuya amesisitiza kuwa Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wananchi kupata huduma za upimaji na urasimishaji wa ardhi kwa gharama zinazozingatia miongozo rasmi ya sekta hiyo.
Ameendelea kuwahimiza wananchi kutumia fursa zinazotolewa na miongozo hiyo kurasimisha na kupima maeneo yao kwa kufuata taratibu halali, ili kuwa na uhakika wa umiliki na matumizi salama ya ardhi.