Habari
Serikali Yaendelea Kutekeleza Maamuzi ya Kutatua Migogoro ya Ardhi Vijijini
- 22 Jun, 2026
Serikali imesema utekelezaji wa maamuzi ya kutatua migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji na mitaa 975 unaendelea katika maeneo mbalimbali nchini huku hatua mbalimbali zikichukuliwa kuhakikisha migogoro hiyo inapatiwa ufumbuzi wa kudumu.
Hayo yameelezwa leo Juni 22, 2026 bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Kaspar Mmuya, wakati akijibu swali la Mhe. Kunti Yusuph Majalla mbunge wa Chemba aliyetaka kufahamu ni lini Serikali itatoa taarifa ya Kamati ya Mawaziri Nane kuhusu migogoro ya ardhi kati ya maeneo ya hifadhi na watumiaji wengine wa ardhi.
Mhe. Mmuya alisema Serikali iliunda Kamati ya Mawaziri Nane wa kisekta kusimamia utekelezaji wa uamuzi wa Serikali kuhusu migogoro ya matumizi ya ardhi iliyohusisha vijiji na mitaa 975 pamoja na maeneo ya hifadhi, mashamba, ranchi za Serikali na vijiji husika.
Alisema Ofisi za Wakuu wa Mikoa zimeendelea kuratibu utekelezaji wa maamuzi hayo kwa kusimamia umegaji wa maeneo yanayorejeshwa kwa wananchi, uthamini wa mali za wananchi wanaopisha shughuli za uhifadhi, ulipaji wa fidia, uwekaji wa alama za mipaka pamoja na uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi.
Aidha, Serikali imeendelea kutenga fedha kwa ajili ya kukamilisha shughuli hizo, huku utekelezaji ukifanyika kwa ushirikiano wa wananchi na mamlaka za Serikali za Mitaa katika maeneo husika.
Hata hivyo Mhe. Mmuya alibainisha kuwa baada ya utekelezaji wa maamuzi hayo kukamilika, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi itawasilisha taarifa husika kwa mamlaka zinazohusika ikiwa ni jitihada za serikali za kumaliza migogoro ya matumizi ya ardhi kati ya wananchi na maeneo ya hifadhi na kuhakikisha usimamizi bora wa ardhi nchini.