Habari

SERIKALI YAENDELEA KUKABILIANA NA MIGOGORO YA ARDHI KIGOMA UJIJI

  • 21 Apr, 2026
SERIKALI YAENDELEA KUKABILIANA NA MIGOGORO YA ARDHI KIGOMA UJIJI

Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeendelea kuchukua hatua madhubuti za kupunguza na kumaliza migogoro ya ardhi kwa kuimarisha mifumo ya utatuzi wa migogoro pamoja na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi sahihi ya ardhi.

Kauli hiyo imetolewa bungeni leo tarehe 17 Aprili 2026 na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Kaspar Mmuya wakati akijibu kujibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe.Naomy Duncan Mwaipopo, aliyetaka kufahamu mikakati ya Serikali katika kutatua migogoro ya ardhi katika Manispaa hiyo.

Mhe. Mmuya amesema jumla ya migogoro ya ardhi 1,092 ilipokelewa na kusajiliwa katika Manispaa ya Kigoma Ujiji, ambapo migogoro 1,046 tayari imetatuliwa kwa njia ya kiutawala, huku migogoro 46 ikiwa katika hatua mbalimbali za utatuzi.

Aidha, Serikali imebainisha kuwa inaendelea kutoa elimu kwa umma ili kuzuia migogoro inayoweza kuepukika, kuwakumbusha watumishi wa sekta ya ardhi kuzingatia sheria, kanuni na taratibu, pamoja na kusimamia nidhamu na maadili ya kazi kwa watumishi hao.

Ameongeza kuwa, kupitia Programu ya Kliniki za Ardhi, wananchi wenye migogoro wamekuwa wakipata fursa ya kukutana moja kwa moja na wataalam pamoja na viongozi kwa ajili ya kusikilizwa na kutatuliwa changamoto zao, hatua inayolenga kuleta haki, utulivu na maendeleo endelevu katika sekta ya ardhi nchini.