Habari
SERIKALI YACHUKUA HATUA MGOGORO WA WAKULIMA NA MWEKEZAJI WA MOROGORO SUGAR
- 09 Apr, 2026
Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeandaa Mipango ya Matumizi ya Ardhi katika vijiji vyote vinavyozunguka mashamba mwekezaji wa kampuni ya Morogoro Sugar yenye ukubwa wa hekta 3,632.25 ili litumike kama ilivyokusudiwa.
Hayo yamesemwa Bungeni 08 Aprili 2026 jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Kaspar Mmuya wakati akijibu swali la Mbunge wa Morogoro Kusini, Mhe. Zuberi Yahya Mfaume, aliyehoji ni lini Serikali itaingilia kati na kudhibiti migogoro ya ardhi kati ya Wakulima na Wawekezaji wa Morogoro Sugar.
Mhe. Mmuya amesema kuwa Wizara imebaini kuwa chanzo kikuu cha msuguano huu ni baadhi ya wananchi kuanza kufanya shughuli mbalimbali ndani ya ardhi ya mwekezaji kinyume cha sheria.
Ameongeza kuwa Serikali imechukua hatua kali za kisheria dhidi ya viongozi wa vijiji ambao wamekuwa wakichochea migogoro hiyo kwa kuwauzia wananchi ardhi ndani ya maeneo ya uwekezaji. Usimamizi huu unalenga kukomesha vitendo vya uuzaji holela wa ardhi ya Serikali na mwekezaji, jambo ambalo limekuwa likisababisha usumbufu mkubwa kwa pande zote mbili.
Serikali imetekeleza mipango ya matumizi ya ardhi na kutoa hati za hakimiliki za kimila kwa wananchi Jirani na eneo la uwekezaji ili kutofautisha maeneo ya kijiji na yale ya mwekezaji.
Hatua nyingine ambazo zimechukuliwa na Wizara ni kuundwa kwa Kamati iliyowashirikisha wananchi wa vijiji husika na viongozi kwa lengo la kutoa mrejesho kwa wananchi kuhusu hatua zilizofikiwa katika utatuzi wa migogoro na wananchi wameendelea kupewa elimu kuhusu umuhimu wa kuheshimu mipango ya matumizi ya ardhi iliyopitishwa.
Mgogoro huo unahusisha mashamba tisa yanayomilikiwa na kampuni ya Morogoro Sugar kupitia TISEZA, yakiwa na hati namba 7317, 7315, na 7311 kwa ajili ya kilimo cha miwa.
Maeneo yanayohusika ni pamoja na vijiji vya Gomero, Nyarutanga, Dakawa, Bwakila Chini, Mngazi, Vigolegole, Msonge, Tanunguo, na Tulo.