Habari

SERIKALI KUWAFUATILIA WADAIWA KODI YA PANGO LA ARDHI

  • 12 May, 2026
SERIKALI KUWAFUATILIA WADAIWA KODI YA PANGO LA ARDHI

Afisa Kodi wa Jiji la Dodoma, Bi. Matilda Mactavo amesema  Serikali itaendelea kuwafuatilia wadaiwa wa kodi ya pango la ardhi katika Jiji la Dodoma pamoja na kuhakikisha maeneo yote ya uwekezaji yanatumika kama ilivyokusudiwa.

 

Bi. Mactavo ambaye ni Afisa Ardhi Mwandamizi katika halmashauri ya Jiji la Dodoma amesema hayo tarehe 11 Mei, 2026 wakati wa ziara ya kikazi iliyohusisha maeneo ya NCC Mlimani, Iyumbu na Njedengwa.

 

"Ulipaji wa kodi ya pango la ardhi ni wajibu wa kila mmiliki wa ardhi. Fedha zinazokusanywa hutumika katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na utoaji wa huduma muhimu kwa wananchi,” amesema Bi. Mactavo.

 

Bi. Mactavo ameoongoza kikosi kazi cha kusambaza Hati za Madai ya Kodi ya Pango la Ardhi katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dodoma.

 

Akigeukia uendelezaji wa maeneo ya uwekezaji Bi. Mactavo amesema, yapo baadhi ya maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji na  yameachwa bila kuendelezwa kwa muda mrefu.

 

Alisisitiza kuwa, maeneo yote yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji yanapaswa kuendelezwa kwa mujibu wa masharti ya hati na kwa kuzingatia sheria za ardhi nchini.

 

Ziara hiyo ni sehemu ya kampeni ya kuhamasisha ulipaji wa kodi ya pango la ardhi pamoja na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kutekeleza wajibu wao wa kisheria na kutumia ardhi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.