Habari

SERIKALI KUTENGA HEKTA MILIONI 6 KWA AJILI YA WAFUGAJI IFIKAPO 2030

  • 04 Sep, 2026
SERIKALI KUTENGA HEKTA MILIONI 6 KWA AJILI YA WAFUGAJI IFIKAPO 2030

Serikali imeeleza kuwa ina lengo la kutenga, kupima na kumilikisha maeneo ya wafugaji yenye ukubwa wa hekta milioni sita (6) nchini kote ifikapo mwaka 2030, ili kuimarisha matumizi bora ya ardhi na kuondoa migogoro ya wakulima na wafugaji.

 

Hayo yamesemwa leo tarehe 04 Septemba 2026 Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Kaspar Mmuya, wakati akijibu swali la Mbunge wa Mbogwe, Mheshimiwa Fagason Aron Nkingwa, aliyehoji kuhusu lini Serikali itatimiza ahadi yake ya kutenga na kumilikisha maeneo kwa ajili ya wafugaji nchini.

 

Mhe. Mmuya alieleza kuwa katika kufanikisha azma hiyo, hadi kufikia mwaka 2025/26, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi iliandaa mipango ya matumizi ya ardhi iliyowezesha kutenga zaidi ya hekta milioni 3.6 kwa ajili ya shughuli za ufugaji.

 

Ameongeza kuwa katika mwaka huo wa 2025/26, zaidi ya hekta milioni 1.3 zilizopo katika vijiji 365 zimepimwa na kutangazwa rasmi kupitia Gazeti la Serikali (GN Na. 597 na 718). 

 

Sambamba na hatua hiyo, mipango ya matumizi ya ardhi imejumuisha maeneo 53 yenye jumla ya hekta 790,865.54, ambapo wananchi wamekabidhiwa Hati za Hakimiliki za Kimila ili kuimarisha umiliki, kusimamia rasilimali hizo kwa ufanisi, na kuongeza upatikanaji wa maeneo ya malisho ya mifugo.

 

Naibu Waziri Mmuya alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kutenga, kupima na kumilikisha maeneo ya malisho kwa ajili ya matumizi ya mifugo kwa kuzingatia mahitaji ya kila eneo nchini.