Habari

SERIKALI KUJA NA SULUHU YA MIGOGORO YA ARDHI NCHINI

  • 06 Jul, 2026
SERIKALI KUJA NA SULUHU YA MIGOGORO YA ARDHI NCHINI

SERIKALI imetangaza mkakati mzito wa kupima na kuweka mipaka ya wazi katika kila kijiji na wilaya nchini kote, ikiwa ni hatua ya kudumu ya kukomesha migogoro ya ardhi inayokwamisha shughuli za kiuchumi na kijamii. 

 

Kauli hiyo imetolewa leo Ijumaa, Julai 3, 2026, na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Kaspar Mmuya alipokuwa akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Uwanja wa Mwenge, wilayani Butiama mkoani Mara, ikiwa ni sehemu ya ziara ya kikazi ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba.

 

Mhe. Mmuya amesema mpango huo unalenga kusimamia kwa ufanisi jumla ya kilometa za mraba 948,132 za ukubwa wa ardhi ya Tanzania ili kuondoa mwingiliano wa matumizi ya rasilimali hiyo adhimu.

 

Amesema kuwa chanzo kikubwa cha migogoro nchini, inatokana na mkanganyiko wa matumizi ya ardhi kati ya watu binafsi, familia, na taasisi mbalimbali ambapo ili kupata ufumbuzi wa kudumu, alifafanua kuwa wizara yake inashirikiana bega kwa bega na halmashauri, wakuu wa wilaya, na wananchi wenyewe ili kubainisha na kusimika alama za msingi zisizofutika za mipaka.

 

"Hatuwezi kuendelea kuruhusu migogoro ya mipaka irudishe nyuma maendeleo ya wananchi wetu. Serikali imejipanga kupima kila kona ya nchi hii ili kila mwananchi atambue haki na mipaka yake ya kisheria na azalishe kwa amani," alisisitiza Naibu Waziri Kaspar Mmuya.

 

Aidha Naibu Waziri Mmuya alifafanua kuwa kila kijiji kitakuwa na mpango madhubuti wa matumizi bora ya ardhi. Alisema kuwa maeneo yatatenganishwa rasmi kwa ajili ya shughuli za kilimo, malisho ya mifugo, makazi mapya, shule, hospitali, pamoja na maeneo ya maziko ili kuzuia muingiliano usio wa lazima hapo baadaye.

 

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Mmuya alitolea ufafanuzi Mgogoro wa ardhi kati ya Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius K. Nyerere cha Kilimo na Teknolojia (MJNUAT) na wananchi wa Butiama unatokana na upanuzi wa miundombinu ya chuo hicho, ambapo amezitaka pande zote mbili kukaa meza moja haraka iwezekanavyo ili kufikia maridhiano kwa kufuata taratibu na sheria za utwaaji wa ardhi.

 

Kadhalika Naibu Waziri Mmuya alitoa wito kwa wananchi kuitazama miradi ya maendeleo kote nchini kama fursa ya kiuchumi, akisema serikali itakutana na wadau wote na wawekezaji ili kufanya mapitio na kuhakikisha wananchi wanapata fidia stahiki, zenye tija, na kwa wakati kulingana na sheria ya uthamini.