Habari

SERIKALI KUIPA NGUVU SEKTA YA NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI

  • 02 Oct, 2026
SERIKALI KUIPA NGUVU SEKTA YA NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI

Serikali imesema imeanza kuweka msisitizo zaidi katika sekta ya nyumba na maendeleo ya makazi ili kuimarisha upatikanaji makazi bora, salama na yenye kuzingatia mipango miji, sheria na viwango vya ujenzi nchini.

 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhandisi Anthony Sanga, amesema sekta hiyo imekuwa ikipewa nafasi ndogo ikilinganishwa na masuala ya ardhi, hivyo kuna umuhimu wa kuongeza nguvu katika kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wake.

 

Amewataka waandishi wa habari nchini kuongeza juhudi katika kuripoti masuala ya nyumba na maendeleo ya makazi ili kuwajengea wananchi uelewa kuhusu fursa zilizopo, changamoto na umuhimu wa kuzingatia sheria, kanuni na viwango vya ujenzi.

 

Mhandisi Sanga ameyasema hayo Oktoba 1, 2026 jijini Dodoma wakati akifungua mkutano wa Jukwaa la Wahariri ulioandaliwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Makazi (UN-Habitat), kuelekea maadhimisho ya Siku ya Makazi Duniani yatakayofanyika Oktoba 5, 2026.

 

"Mara nyingi tumekuwa tukijikita zaidi kwenye taarifa za ardhi pekee, lakini taarifa za nyumba na maendeleo ya makazi zimekuwa haziripotiwi kwa kiwango kikubwa," amesema

 

Ameeleza kuwa, Wizara itaendelea kushirikiana na wanahabari kwa kuhakikisha wanapata taarifa sahihi na kwa wakati kuhusu sekta hiyo, zikiwemo fursa za uwekezaji, changamoto zinazojitokeza na hatua zinazochukuliwa katika kuzitatua ili waweze kuifikishia jamii elimu yenye tija.

 

Amesema, ushirikiano kati ya Serikali na vyombo vya habari ni muhimu kutokana na kasi ya ukuaji wa miji na ongezeko la watu, vinavyochochea mahitaji ya ardhi, nyumba, miundombinu na huduma za msingi.

 

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania, Dk. Mary Kafyome, amesema vyombo vya habari vina wajibu wa kutoa taarifa zinazowawezesha wananchi kuelewa masuala mbalimbali ya maendeleo ya miji na makazi.

 

Ametaja masuala ya ujenzi wa barabara, upimaji wa maeneo na maendeleo ya nyumba kuwa miongoni mwa maeneo yanayohitaji kupewa kipaumbele katika uripoti wa habari ili wananchi wafahamu umuhimu wa miradi hiyo, fursa zinazotokana nayo, changamoto zake na nafasi yao katika kuchangia maendeleo ya miji.

 

Naye Afisa Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Makazi (UN-Habitat) nchini Tanzania, Grace Lubaale, amesema, mkutano huo ni hatua ya kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, vyombo vya habari na wadau wengine katika kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi na kwa wakati kuhusu maendeleo ya miji na makazi.

 

Amesema, ushirikiano huo utasaidia kuongeza uelewa wa jamii kuhusu masuala ya makazi na maendeleo endelevu ya miji.

 

Tanzania itaungana na nchi nyingine duniani kuadhimisha Siku ya Makazi Duniani Oktoba 5, 2026, ikiwa na kaulimbiu isemayo “Makazi Toshelevu kwa Wote.”