Habari

SAMIA ARDHI KLINIKI YALETA TABASAMU SINGIDA: WANAWAKE ZAIDI YA 50 WAPEWA HATI MILIKI NA KUHIMIZWA KUMILIKI ARDHI

  • 09 Mar, 2026
SAMIA ARDHI KLINIKI YALETA TABASAMU SINGIDA: WANAWAKE ZAIDI YA 50 WAPEWA HATI MILIKI NA KUHIMIZWA KUMILIKI ARDHI

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhandisi Antony Sanga, amegawa zaidi ya hati miliki 50 za ardhi kwa wanawake mkoani Singida kupitia zoezi la Samia Ardhi Kliniki, huku akiwahamasisha wanawake kujitokeza kumiliki ardhi ili kujiletea maendeleo binafsi na ya familia zao.

 

Akizungumza Machi 5, 2026 katika Ofisi ya Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Singida, Mhandisi Sanga amesema Wizara ya Ardhi chini ya Waziri Dkt. Leonard Akwilapo imejipanga kuongeza idadi ya wanawake wanaomiliki ardhi nchini kwa kuendelea kutoa elimu na huduma za ardhi kwa wananchi.

 

Amesema Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995 (Toleo la 2023) inatoa haki sawa kwa wanawake na wanaume kumiliki ardhi, hivyo wizara inaendelea kuhamasisha utekelezaji wake na kuwataka watumishi wa sekta ya ardhi nchini kuhakikisha wanawake wanapata huduma bila ubaguzi.

 

Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Singida Bi. Shamim Hoza amesema kupitia Samia Ardhi Kliniki, wanawake 144 na wanaume 36 wamepatiwa huduma mbalimbali za ardhi, migogoro 18 imepokelewa na 10 kutatuliwa, viwanja 18 vimepimwa, zaidi ya milioni 23 zimekusanywa kama ada na hati Zaidi ya 50 zimetolewa wanawake huku zaidi ya wanawake 1,350 wakipatiwa elimu ya masuala ya ardhi.

 

Naye Mkuu wa Wilaya ya Singida Godwin Gongwe, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa Halima Dendego, amesema ujio wa Samia Ardhi Kliniki ni muhimu kwani zaidi ya kesi 900 za ardhi zimeanza kushughulikiwa kupitia Kikosi Kazi cha SAMIA, huku akibainisha kuwa wanawake ndio waathirika wakubwa wa migogoro ya ardhi hivyo wanahitaji kuendelea kupewa elimu na haki zao.

 

 Akizungumza kwaniaba ya wanawake walioshiliki samia Ardhi kliniki Mkoani Singida Bi Aisha Mohamed emeishukuru wizara ya Ardhi kwa kuwaletea Samia Ardhi Kliniki mkoa wa Singida kwaani imewanufaisha wanawake wengi kupitia  upimaji wa maeneo yao,kupatiwa Hati miliki  na kuwaongezea uelewa kuhusu masuala ya Miliki za Ardhi.

 

Kamishna Mkuu Msaidizi wa Ardhi Bw. Hussein Sadiki, Katibu Tawala Msaidizi upande wa Miundombinu Bw. Kirina Domicianus aliyemwakilisha Katibu Tawala wa Mkoa ni miongoni Viongozi walioshiriki Hafla ya Ugawaji wa Hati na utoaji wa elimu ya Masuala ya Ardhi katika Samia Ardhi Kliniki Mkoani Singida.