Habari
RC MOROGORO AWAAPISHA WAZEE WATATU KUTUMIKIA BARAZA LA ARDHI MVOMERO
- 18 Sep, 2026
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Queen Sendiga, amewaapisha wazee watatu watakaohudumu katika Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Mvomero, hatua inayolenga kuendelea kuimarisha utendaji wa mabaraza hayo na kuongeza ufanisi katika kushughulikia migogoro ya ardhi.
Akizungumza wakati wa kuwaapisha wazee hao tarehe 17 septemba 2026, Mhe. Sendiga amewataka kutekeleza majukumu yao kwa hekima, uadilifu na haki, kwa kuzingatia sheria na taratibu katika kusikiliza na kutatua migogoro ya ardhi inayowasilishwa mbele ya baraza.
Amesema mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya ni sehemu muhimu ya mfumo wa utoaji haki katika masuala ya ardhi, hivyo wajumbe wake wanapaswa kutambua dhamana waliyopewa na kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati.
“Nendeni mkasimamie haki, msikilize pande zote kwa usawa na mfanye kazi kwa hekima na uadilifu,” amesema Mhe. Sendiga.
Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Morogoro, Idrisa Kayera, amesema wazee wanaohudumu katika mabaraza ya ardhi wameendelea kuwa chachu katika kusaidia Serikali kukabiliana na migogoro ya ardhi katika maeneo mbalimbali.
Kayera amesema wazee hao pia wamekuwa wakisaidia katika kutoa elimu kwa wananchi, kusikiliza changamoto zao na kushiriki katika juhudi za kusuluhisha migogoro ya ardhi, hivyo kuchangia katika kuimarisha amani na utulivu katika jamii.
Amesema Serikali itaendelea kuimarisha mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya ili yaweze kutekeleza ipasavyo jukumu lake la kusaidia wananchi kupata haki na suluhu za migogoro ya ardhi kwa kuzingatia sheria.
Uapisho huo ni sehemu ya hatua zinazoendelea kuchukuliwa katika kuimarisha mabaraza ya Ardhi na Nyumba katika halmashauri mbalimbali mkoani Morogoro, kwa lengo la kuongeza ufanisi katika utoaji wa haki na utatuzi wa migogoro ya ardhi.