Habari
RASIMU YA MPANGO WA UENDELEZAJI SINZA YAWASILISHWA KWA WANANCHI
- 21 Sep, 2026
Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu Rasimu ya Mpango wa Uendelezaji Eneo la Sinza, Jijini Dar es Salaam, unaolenga kuendana na mabadiliko ya maendeleo ya eneo hilo pamoja na mahitaji ya kizazi kijacho.
Timu ya Wizara ya Wizara ya Ardhi ikiongozwa na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Makazi, Deogratius Kalimenze, imekutana na wakazi wa Sinza D na kutoa elimu kuhusu rasimu hiyo, huku wananchi wakipewa fursa ya kuuliza maswali, kutoa maoni na kueleza hofu zao kuhusu utekelezaji wa mpango huo.
Kalimenze amesema mabadiliko ya kasi ya ukuaji wa miji na maendeleo yaliyotokea katika maeneo yaliyopangwa miaka mingi iliyopita yameifanya Serikali kuona umuhimu wa kupitia upya mipango hiyo ili iendane na mahitaji ya sasa na ya miaka ijayo.
Ameeleza kuwa, uamuzi wa kuipanga upya Sinza umetokana na makubaliano ya Baraza la Madiwani la Manispaa ya Ubungo, huku akieleza kuwa mpango huo umeandaliwa kwa mtazamo wa maendeleo ya kipindi cha miaka 20.
“Hali ya mipango miji iliyopangwa miaka mingi iliyopita imebadilika, ndiyo maana Serikali ilikubaliana mji wa Sinza upangwe upya na kuwa eneo la mpango mpya wa uendelezaji,” amesema Kalimenze.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo wa Maendeleo ya Makazi, mipango ya aina hiyo imeandaliwa pia katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam, yakiwemo Kinondoni, Kariakoo, Buguruni, Ilala na City Centre, huku maeneo mengine yakiendelea kufanyiwa mipango.
Kalimenze pia amefafanua kuwa mpango huo hauondoi umiliki wa ardhi wa wananchi, akisema lengo lake ni kuweka utaratibu wa matumizi ya ardhi unaoendana na mahitaji ya maendeleo ya eneo hilo.
“Mtekelezaji mkuu wa mpango ni mdau mwenyewe ambaye ni mmiliki wa ardhi hapa Sinza. Hali ya umiliki haiondolewi kwa mpango huu, ila matumizi yanaweza kubadilishwa kulingana na mahitaji, kama biashara au shughuli nyingine za kijamii,” amesema.
Baadhi ya wakazi waliochangia maoni yao walieleza hofu kuhusu namna wamiliki wa ardhi watakavyoweza kukubaliana na wawekezaji, huku wakitaka Serikali iwe sehemu ya makubaliano hayo ili kulinda maslahi ya wananchi.
Akijibu hoja hiyo, Kalimenze amesema makubaliano ya kibiashara kati ya wamiliki wa ardhi na wawekezaji si sehemu ya mpango wa uendelezaji, hivyo Serikali haitahusika katika kuamua namna wamiliki na wawekezaji watakavyokubaliana kuhusu malipo au masharti ya uwekezaji.
Amesema jukumu la mpango huo ni kuainisha matumizi ya ardhi na kuweka mwelekeo wa uendelezaji wa eneo, hatua ambayo itarahisisha utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo katika Sinza.
Amewataka wakazi wa Sinza kushiriki kikamilifu katika mchakato huo kwa kutoa maoni na mapendekezo yao ili kusaidia kuandaa mpango unaozingatia mahitaji ya wananchi, mabadiliko ya eneo hilo na maendeleo endelevu kwa kipindi kijacho.