Habari
RAIS SAMIA MGENI RASMI UZINDUZI WA SERA YA TAIFA YA ARDHI
- 15 Mar, 2025

WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi itazindua rasmi Sera ya Taifa ya Ardhi ya Mwaka 1995 toleo la mwaka 2023, Machi 17, 2025 katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Center jijini Dodoma ambapo mgeni rasmi katika uzinduzi huo atakua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza na wandishi wa habari jijini Dodoma leo tarehe 15 Machi, 2025, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Deogratius Ndejembi amesema maandalizi ya uzinduzi huo yamekamilika ambapo kauli mbiu kwenye uzinduzi huu wa Sera ya Taifa ya Ardhi ya Mwaka 1995 toleo la mwaka 2023 ni “ Sera ya Ardhi-Msingi wa Ustawi na Maendeleo Endelevu ya Taifa.”
“ Nichukue fursa hii kuwakaribisha wadau wa sekta ya ardhi, washirika wa kimaendeleo, viongozi mbalmbali wa vyama na Serikali, wanahabari na watanzania wote kwa ujumla kushiriki katika tukio hili la kihistoria.
Tunatarajia uzinduzi huu wa sera kuhudhuriwa na wageni zaidi ya 3000 na hafla hiyo itafanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete kuanzia saa 1:00 asubuhi. Tukio hili pia litarushwa mbashara kupitia Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na vyombo mbalimbali vya habari lengo likiwa kuhakikisha watanzania wote wanashiriki,” Amesema Mhe. Ndejembi.
Kwa mujibu wa GN Na. 385 ya Mei 07, 2021 na marekebisho yake kupitia GN Na. 534 ya Julai 02, 2021 pamoja na majukumu mengine, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ndiyo yenye dhamana ya kusimamia sekta ya ardhi nchini.