Habari

RAIS DKT. SAMIA AITAKA WIZARA YA ARDHI KUENDELEZA KLINIKI ZA ARDHI NA KUONGEZA KASI YA UPIMAJI

  • 27 Nov, 2026
RAIS DKT. SAMIA AITAKA WIZARA YA ARDHI KUENDELEZA KLINIKI ZA ARDHI NA KUONGEZA KASI YA UPIMAJI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameitaka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuendeleza na kuimarisha Kliniki za Ardhi kwa kuhakikisha zinawafikia wananchi katika maeneo yao, kusikiliza changamoto zinazohusu ardhi na kuzitatua kwa wakati ili kuzuia migogoro inayoweza kuhatarisha amani na usalama wa wananchi.

 

Rais Dkt. Samia amesisitiza kuwa Kliniki za Ardhi ni njia muhimu ya kusogeza huduma karibu na wananchi, hivyo amemtaka Waziri wa Ardhi kuhakikisha programu hiyo inaendelezwa na kuimarishwa kwa kuwafikia wananchi, kubaini changamoto zao na kuzitafutia ufumbuzi. Ameelekeza kuwa migogoro ya ardhi inapaswa kushughulikiwa mapema ili kuepusha wananchi kufikia hatua ya kuuana kutokana na migogoro hiyo.

 

Aidha, Rais Dkt. Samia ameitaka Wizara kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya upimaji wa ardhi nchini, akibainisha kuwa pamoja na uwepo wa miradi mbalimbali ya upimaji, bado kuna haja ya kuongeza kasi ya utekelezaji wake ili wananchi wengi zaidi wanufaike na huduma hiyo. 

 

Amesisitiza kuwa maeneo yanapokuwa yamepimwa, ni lazima mipaka na umiliki wake viheshimiwe kwa mujibu wa sheria.

 

Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia amekemea vitendo vya baadhi ya watumishi wasio waaminifu wanaohusika na utoaji wa viwanja kwa watu zaidi ya mmoja, akisisitiza umuhimu wa uadilifu, uwajibikaji na usimamizi madhubuti katika utoaji wa huduma za ardhi ili kulinda haki za wananchi na kuzuia migogoro inayotokana na vitendo hivyo.

 

Maelekezo hayo ameyatoa leo, Novemba 27, 2026, Ikulu jijini Dar es Salaam, baada ya kumuapisha Mhe. David Silinde kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, akimtaka kutekeleza majukumu yake kwa kuhakikisha changamoto za wananchi katika sekta ya ardhi zinapatiwa ufumbuzi na huduma za ardhi zinaboreshwa kwa manufaa ya wananchi na maendeleo ya taifa.