Habari
PROF. SHEMDOE AAGIZA WIZARA YA ARDHI KUONGEZA MUDA WA KLINIKI, ZAIDI YA WANANCHI 1,300 WANUFAIKA NA KLINIKI HIYO YA ARDHI
- 24 Jun, 2026
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Prof. Riziki Shemdoe wakati akifunga maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma kwa mwaka 2026 kama Mgeni Rasmi, ametembelea banda la Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na kupongeza kasi ya utoaji wa huduma huku akitoa maagizo mazito kuhusu matumizi ya mifumo ya kidijitali.
Akiwa kwenye banda hilo, Waziri Shemdoe amewaelekeza wataalamu na watendaji wa sekta ya ardhi kuongeza muda wa kutoa huduma hadi tarehe 30 mwezi huu ili kuhakikisha wananchi wote wanaozunguka kupata huduma wanatuliwa kero zao kabla ya kufunga rasmi kliniki hizo za ardhi.
“Sasa maelekezo yangu hawa wa ardhi wabaki hapa mpaka tarehe 30 ili hawa wote wanaozungujka hapa waje wapewe huduma” alisema Waziri Prof. Riziki Shemdoe
Katika hatua nyingine Waziri huyo amewataka wataalamu wa Ardhi nchini kuendelea kutumia mifumo ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi hasa katika mchakato wa kufuatilia hati.
"Mimi leo nimekuwa mgeni rasmi wa kufunga Wiki ya Utumishi, ninawaelekeza: mahali popote ambapo mifumo inatakiwa itumiwe, itumiwe mifumo," alisisitiza Waziri Shemdoe huku akibainisha kuwa changamoto kubwa iliyopo nchini kwa sasa ni masuala ya ardhi, na uwepo wa kliniki hizo unaleta faraja na tabasamu kwa wananchi.
Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Dodoma Bw. Geofrey Mwamusojo ameeleza kuwa hadi sasa banda hilo limefanikiwa kuwahudumia wananchi 1,306 waliokuwa na mahitaji mbalimbali, ikiwemo ushauri wa kisheria na utatuzi wa migogoro. Kati yao, wananchi 310 wamefanikiwa kukabidhiwa hati zao za miliki papo hapo.
Nao wananchi waliopata fursa ya kupata hati zao kwa haraka wamepongeza juhudi hizo, wakieleza kufurahishwa kwao na weledi wa watendaji wa sekta ya ardhi.
"Nimefurahi sana kupata hati katika siku ya leo. Sijachukua muda mrefu, nimeanza mchakato kama majuzi na leo nimefanikiwa kuipata," alisema Robert Michael
Naye Bi. Kibibi Shaban aliongeza kwa kuwasihi wananchi wenzake kuwa wavumilivu na kuhakikisha wanarasimisha maeneo yao, hususan wanaponunua viwanja vipya ili kuwa na usalama wa miliki zao.