Habari

PINDA AWAFUNDA WATENDAJI WA SEKTA YA ARDHI MWANZA

  • 30 Jan, 2024
PINDA AWAFUNDA WATENDAJI WA SEKTA YA ARDHI MWANZA

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe Geophrey Pinda amewafunda watendaji wa sekta ya ardhi katika jiji la Mwanza kwa kuwataka kusimamia sekta hiyo kwa kuzingatia kanuni, taratibu na miongozi ya sekta hiyo.

 

Amesema, kwa kufanya hivyo Wizara ya Ardhi itaweza kuepukana na migogoro ya ardhi isiyo na lazima aliyoieleza kuwa imeendelea kuibuka kila kukicha katika maeneo mbalimbali.

 

Mhe Pinda alisema hayo tarehe 29 Januari 2024 alipokutana na wakuu wa idara na vitengo wanaosimamia sekta ya ardhi katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza pamoja na wale wa Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Mwanza akiwa katika ziara yake mkoani humo.

 

"Ninyi ndiyo wasimamizi wa sekta hii ya ardhi katika jiji la Mwanza hivyo mnao wajibu mkubwa wa kufuata kanuni, taratibu na miongozo ya sekta hii ili kuepusha migogoro ya ardhi" alisema mhe. Pinda

 

Amewataka wakuu hao wa idara na vitengo kuwa washauri wazuri wa wakurugenzi wa halmashauri zao ikiwemo kuzishauri halmashauri kuwa na benki za ardhi katika maeneo yake.

 

"Ninachotaka kuwaambia silka yangu ni kuwapitisha katika maeneo mnayoyasimamia na hii itawasaidia kutekeleza majukumu yenu kwa ufasaha"alisema Mhe. Pinda.

 

Aidha, Naibu Waziri wa Ardhi amehimiza suala la upendo miongoni mwa watumishi wakati wote wa utendaji kazi kwa kuwa ndiyo njia pekee ya kuwawezesha wakuu hao wa idara na vitengo kufanya kazi bila kulaumiwa.