Habari

PINDA AELEKEZA MAAFISA ARDHI KUREJESHA MAWE YA MPAKA WA MONDULI NA LONGINDO

  • 24 Jan, 2025
PINDA AELEKEZA MAAFISA ARDHI KUREJESHA MAWE YA MPAKA WA MONDULI NA LONGINDO

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda amewaelekeza maafisa ardhi katika wilaya ya Monduli na Longido kushiriki kikamilifu katika zoezi la kurejesha mawe ya mpaka ya wilaya hizo mbili yaliyong'olewa na kupoteza utambuzi wa mpaka huo.

Naibu Waziri Pinda amesema hayo Januari 23, 2025 katika hafla ya Uzinduzi wa Ulipaji Fidia ya Mradi wa Magadi Soda iliyofanyika katika kata ya Engaruka Wilaya ya Monduli mkoani Arusha.

"Nielekeze Maafisa Ardhi wote wa wilaya zote mbili mguu wa Mkuu wilaya utakaposimama maofisa wote muwepo kwenye kazi ya kurejesha yale mawe ndani ya muda walioahidi" amesema Naibu Waziri Pinda.

Aidha, Naibu Waziri Pinda amemwelekeza Katibu Mkuu Wizara hiyo Mhandisi Anthony Sanga kuziwezesha wilaya hizo kuwa katika mpango wa matumizi bora ambao utahusisha ugawaji wa hati miliki za ardhi.

Awali Wakuu wa Wilaya za Monduli na Longido Mhe. Festo Kiswaga na Mhe. Salum Kali wameahidi mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Makonda kuwa watarejesha mawe ya mpaka huo ifikapo Jumatatu ya Januari 27, 2025.

Urejeshwaji wa mawe ya mpaka utasaidi kumaliza mgogoro huo uliodumu kwa muda mrefu ili wananchi wa wilaya hizo mbili waweze kuendelea na shughuli zao za kila siku ili kujiletea maendeleo yao.