Habari

OFISI YA KAMISHNA WA ARDHI MWANZA YACHUKUA HATUA KUBORESHA HUDUMA ZA ARDHI ILEMELA

  • 21 Apr, 2026
OFISI YA KAMISHNA WA ARDHI MWANZA YACHUKUA HATUA KUBORESHA HUDUMA ZA ARDHI ILEMELA

Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Mwanza imetangaza mpango maalum wa kuboresha utoaji huduma za sekta ya ardhi katika Manispaa ya Ilemela jijini Mwanza kufuatia malalamiko yaliyojitokeza hivi karibuni kuhusu ucheleweshaji na usumbufu wa huduma katika ofisi za manispaa hiyo.

 

Akitoa taarifa ya mpango huo, Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Mwanza Bw. Wilson Luge amesema, tayari ofisi yake umechukua hatua za haraka kushughulikia changamoto zilizobainishwa ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa uwazi, weledi na kwa wakati.

 

Kwa mujibu wa Bw. Luge, hatua hizo zimeanza kwa kufanyika kwa kikao maalum kilichowakutanisha wataalam wote wa sekta ya ardhi katika Manispaa ya Ilemela, ambapo walijadili kwa kina vyanzo vya changamoto hizo pamoja na kuweka mikakati ya kuboresha utoaji huduma kwa ufanisi zaidi.

 

Katika maboresho hayo, matumizi ya mfumo wa kidijiti wa e-Ardhi yamepewa kipaumbele, kutokana na ukweli kuwa takribani asilimia 95 ya huduma za ardhi zinatolewa kupitia mfumo huo.

 

Katika kuongeza ufanisi taarifa hiyo imeweka wazi kuwa, watumishi zaidi ya 30, wakiwemo wanafunzi wanaofanya mafunzo kwa vitendo, wanatarajiwa kuanzia Aprili 20, 2026 kushuka hadi ngazi ya kata, hususan Buswelu na Kahama, kwa lengo la kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi ya mfumo huo pamoja na kuwahudumia moja kwa moja.

 

Aidha, menejimenti ya Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Mwanza imeelekeza maombi yote ya huduma yatakayowasilishwa nje ya mfumo wa e-Ardhi yatapatiwa majibu ya maandishi ndani ya siku saba za kazi. Pia, miamala yote iliyopokelewa hadi Aprili 17, 2026 inapaswa kuwa imefanyiwa kazi ifikapo Aprili 21, 2026.

 

Katika hatua nyingine ya kuimarisha uwajibikaji, taarifa hiyo imeelezwa kuwa kila siku ya Alhamisi ya wiki, Kamishna wa Ardhi Mkoa pamoja na wakuu wa vitengo watafanya kazi kwa pamoja katika ofisi za Manispaa ya Ilemela na Jiji la Mwanza ili kutoa huduma kwa wananchi kwa karibu zaidi.

 

Vile vile, wananchi watakaohitaji kuwakilishwa katika kufuatilia huduma zao wanalazimika kuwa na nyaraka halali ya kisheria ya uwakilishi (Power of Attorney) iliyosajiliwa, ili kuhakikisha uwazi na uhalali wa huduma zinazotolewa.

 

Wakati huo huo, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupitia Katibu Mkuu wake inaendelea na uchunguzi wa kina kubaini watumishi wanaosababisha usumbufu katika utoaji wa huduma. Imeelezwa kuwa, hatua kali za kisheria na kiutumishi zitachukuliwa dhidi ya wote watakaobainika kukiuka taratibu.