Habari

OFISI YA ARDHI MWANZA YAENDELEA KUTOA HUDUMA KWA WANANCHI KUPITIA MFUMO WA e-ARDHI

  • 29 Sep, 2026
OFISI YA ARDHI MWANZA YAENDELEA KUTOA HUDUMA KWA WANANCHI KUPITIA MFUMO WA e-ARDHI

Kupitia maboresho makubwa yanayoendelea kufanyika katika mifumo ya Sekta ya Ardhi, Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Mwanza imeendelea kutoa huduma kwa ufanisi kwa wananchi wanaotembelea Kliniki ya Ardhi katika eneo la Misungwi–Usagara mkoani Mwanza.

 

Akizungumza wakati wa Kliniki hiyo, Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Mwanza, Bw. Wilson Luge, amesema kuwa matumizi ya Mfumo wa e-Ardhi yameendelea kurahisisha upatikanaji wa huduma za ardhi kwa wananchi, ambapo mwananchi anaweza kuanzisha muamala wa ardhi akiwa nyumbani bila kulazimika kufika ofisini.

 

Aidha, Kamishna huyo amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi katika Kliniki ya Ardhi ili kupata elimu na uelewa wa namna ya kutumia mfumo huo, unaolenga kusogeza huduma za ardhi karibu zaidi na wananchi na kurahisisha upatikanaji wa huduma.

 

Ameongeza kuwa, mbali na elimu kuhusu matumizi ya e-Ardhi, wananchi wanaotembelea Kliniki hiyo wanapata fursa ya kupata elimu kuhusu masuala mbalimbali ya ardhi, ikiwemo umuhimu wa umiliki wa ardhi kwa pamoja baina ya wanandoa pamoja na masuala ya umiliki wa ardhi kwa wanawake.

 

Kliniki ya Ardhi inaendelea katika mikoa yote ya Tanzania Bara na inatarajiwa kuhitimishwa tarehe 3 Oktoba 2026.