Habari
OFISI YA ARDHI MJI IFAKARA YAPATIWA VIFAA VYA TEHAMA KUBORESHA UTENDAJI
- 04 Mar, 2026
Ofisi ya Ardhi ya Halmashauri ya Mji Ifakara, mkoani Morogoro, imepatiwa vifaa vya TEHAMA kwa lengo la kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi. Hatua hiyo inakwenda sambamba na utekelezaji wa programu ya Samia Ardhi Kliniki inayoendelea katika halmashauri hiyo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kliniki hiyo iliyofanyika tarehe 3 Machi 2026 katika Ofisi ya Kata ya Viwanja Sitini, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Mhe. Wakili Dunstan Kyobya, alisema kuwa ujio wa vifaa hivyo utaimarisha utunzaji wa kumbukumbu, kuharakisha utatuzi wa migogoro ya ardhi na kurahisisha utoaji wa hatimiliki kwa wakati kupitia mifumo ya kidijitali.
Vifaa hivyo ni sehemu ya mgao wa vifaa 1,429 vyenye thamani ya shilingi bilioni 5.2 vilivyokabidhiwa kwa ofisi za ardhi nchini na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo, tarehe 23 Januari 2026 jijini Dodoma.
Mpango huo ni miongoni mwa juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuimarisha sekta ya ardhi na kusogeza huduma karibu na wananchi.
Samia Ardhi Kliniki inaendelea hadi tarehe 7 Machi 2026 kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, huku wananchi wakihimizwa kujitokeza kwa wingi kupata huduma za Ardhi.