Habari
NDEJEMBI AAGIZA KUWEKWA WAZI TARATIBU ZA KUPATA HATI MILKI OFISI ZOTE ZA ARDHI
- 12 Nov, 2024

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Deogratius Ndejembi ameagiza kuwekwa utaratibu ulio wazi wa kupatiwa Hati Milki za Ardhi katika ofisi zote za ardhi ili wananchi wazifahamu na kuepukana na usumbufu wa upatikanaji hati hizo kwa visingizio mbalimbali.
Mhe. Ndejembi ametoa agizo hilo leo tarehe 11 Novemba 2024 wakati wa kikao kazi cha viongozi na watendaji wa sekta ya ardhi kilichofanyika jijini Dodoma.
Ameweka wazi kuwa, hatasita kuchukua hatua kwa mtumishi yeyote atakayechelewesha utoaji wa hati kama mwananchi anayeoomba hati anazo nyaraka zote na kukamilisha taratibu za kupatiwa hati.
"Mwananchi amekamilisha taratibu zote za kupatiwa hati lakini anazungushwa ila akituma ujumbe kwa waziri na ujumbe huo kutumwa kwa afisa anayehusika basi hati inatolewa" amesema.
Amesema, suala la utoaji Hati Milki za Ardhi kwa sasa lisiwe mjadala na mwananchi mwenye nyaraka zote za kupatiwa hati apatiwe ndani ya wiki moja na kama utaratibu haufahamiki basi kila ofisi kuanzia halmashauri mpaka makao makuu ya wizara kuwe na itaratibu ulio wazi unaoonesha taratibu zote za kupatiwa hati.
"Huenda yanatengenezwa mazingira ya kupenyeza rupia, sisemi kama inafanyika hivyo ila ninasema mtu aliyekamilisha nyaraka zote apate hati ndani ya wiki moja" amesema Mhe Ndejembi.
Aidha, Waziri huyo wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi amewataka watendaji wa sekta ya ardhi nchini kutumia ujuzi na utaalamu walio nao katika kuhudumia wananchi pasipo kufanya uonevu wa aina yoyote na kusisitiza kuwa ofisi yake haitasita kumchukulia hatua mtumishi yoyote atakayepindisha taratibu na kumuonea mtu.
Kupitia kikao hicho na watendaji wa sekta ya ardhi, Mhe. Ndejembi amewataka watendaji hao kutowahudumia wananchi kwa kuangalia hali zao na badala yake wafanye kazi kwa kutenda haki.
"Natamani kuanzishwa kituo cha kuwasilisha malalamiko ambapo wananchi watawasilisha malalamiko yao ya ardhi, tupate namba ya simu ili wananchi wapige simu na kutoa malalamiko yao ya ardhi" amesema Mhe. Ndejembi.
Kikao cha siku mbili cha Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na watendaji wa sekta ya ardhi kina lengo la kufanya tathmini, kuangalia mafanikio pamoja na changamoto na namna ya kukabiliana nazo ili majukumu ya sekta ya ardhi yaweze kutekeleza kwa ukamilifu.