Habari

NAIBU WAZIRI PINDA ATAKA BUSARA KUTATUA CHANGAMOTO ZA SEKTA YA ARDHI

  • 14 Mar, 2024
NAIBU WAZIRI PINDA ATAKA BUSARA KUTATUA CHANGAMOTO ZA SEKTA YA ARDHI

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe, Geophrey Pinda amewataka watumishi wa sekta ya ardhi nchini kutumia busara wakati wote wa kushughulikia changamoto za sekta ya ardhi.

 

Mhe, Pinda ametoa kauli hiyo leo tarehe 11 Machi 2024 wakati wa uzinduzi wa Klinik ya Ardhi katika mkoa wa Mwanza ilinayofanyika viwanja vya Nyamagana

 

''Busara itutangulie wakati tunaenda kutatua migogoro ya ardhi tusimuangalia mtu kwa hali yake bali tumuangalie kwa haki yake'' alisema Mhe, Pinda

 

Amesema, watendaji wa sekta ya ardhi wasiposimamia katika kuwatafutia haki wananchi watasababisha malalamiko yasiyo na tija lakini pia hawataifariji nchi na badala yake watatengeneza malalamiko.

 

Amewaambia watumishi kuwa, kwa namna Wizara ya ardhi inavyofanya  mabadiliko yakiwemo yale ya kimfumo hakutakuwa na nafasi kwa mtu atakayeharibu eneo moja kuhamishiwa eneo lingine.

 

Amewaasa watendaji wa ardhi kufuata sheria na kuwa na maadili mema wakati wote wa kutekeleza majukumu yao pamoja na kujiepusha kabisa vitendo vya rushwa. ''Zingatieni mabadiliko ya sayansi na teknolojia kwa kuwa Wizara yetu ndiko inakoelekea. Pia mdumishe amani, upendo na ushirikiano wakati wa kutekeleza majukumu yenu

 

Aidha, Naibu Waziri wa Ardhi ameitaka Ofisi ya Aradhi mkoa wa Mwanza kuhakikisha inaharakisha utoaji hati milki za ardhi na kuongeza kuwa wizara yake haitasita kumchukulia hatua mtumishi yeyote atakayekwamisha kazi hiyo.

 

Kwa mujibu wa Mhe, Pinda, Wizara ya Ardhi inakamilisha Maboresho ya mfumo wa TEHAMA utakaoruhusu huduma na miamala ya sekta ya ardhi kutolewa kidigitali. Mfumo huo utaanza kutumika hivi karibuni kwa kuanza na mikoa ya Arusha, Tanga, Mwanza na Mbeya.

 

Amempongeza Mhe, Dkt Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuiwezesha Wizara yetu kufanikisha miradi mbalimbali inayoenda kuondoa changomoto katika sekta ya ardhi. Hakika huyu ni Mama wa kipekee na Mungu ampe maisha marefu.

 

Akielezea zaidi kuhusu Klinik aliyoizindua, Naibu Waziri wa Ardhi amesema uzinduzi wa Kilink hiyo ni  muendeleo wa Klinik za Ardhi zilizofanyika maeneo mbalimbali nchini hususan katika majiji makubwa kama vile Dar es Salaam na Dodoma.

 

''Kufanyika kwa Klinik za Ardhi kunatoa fursa kwa wananchi walioshindwa kupata huduma ya sekta ya ardhi katika ofisi zetu za ardhi kwenye halmashauri na mkoa kupata suluhu za changamoto zao ndani ya muda mfupi kwa kuwa Maafisa kutoka idara na vitengo vyote vya sekta ya ardhi kama vile Utawala wa Ardhi, Mipango Miji, Upimaji na Ramani, Uthamini, Msajili wa Hati na Nyaraka pamoja na Mabaraza ya Ardhi wanakuwepo mahala pamoja.

 

Kwa upande wake Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Mwanza Hapiness Mtutwa amesema, Ofisi yake imekuwa ikifanya juhudi mbalimbali kushughulikia changamoto za sekta ya ardhi na hadi kufikia machi mwaka huu wamefanikiwa kutatua migogoro 86 ya ardhi jambo alilolieleza kuwa ni hatua kubwa kwa mkoa wake.

 

Klinik ya Ardhi katika mkoa wa Mwanza itafanyika kwa muda wa Siku saba (7) hadi tarehe 17 March, 2024 hivyo tunaomba ushirikiano wako.

 

Katika hatua nyingine Mkuu wa mkoa wa Mwanza Amos Makalla amemkabidhi Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe, Geophrey Pinda kitabu chenye malalamiko ya Ardhi yaliyoshughulikiwa na mkoa wake.

 

Makabidhiano ya kitabu hicho yamefanyika leo tarehe 11 Machi 2024 katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza wakati wa ziara ya Mhe, Pinda kuzindua  Klinik ya Ardhi katika mkoa huo.

 

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo Mhe, Pinda alipongeza mkuu wa mkoa wa Mwanza kwa juhudi zake za kushughulikia migogoro ya ardhi na kuweka kumbukumbu za kero alizoshughulikia.

 

''Mikoa mingine ingeiga mfano wa mkoa wa Mwanza tungekuwa hatuna kazi kubwa kwa kuwa kutakuwa na kumbukumbu na katika mikoa. Kumbukumbu zitasaidia kupitia wale waliowasilisha migogoro.

 

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Amos Makala amesema, ni vizuri wizara ya ardhi pale inapokuta mkoa umefanya maamuzi kuhusiana na migogoro ya ardhi na wizara kupelekewa tena malalamiko basi ni vizuri  ikarudi mkoa husika kuulizia ama kufanya mawasiliano kwa nia ya kutafuta njia nzuri ya kushughulikia mgogoro.

 

''Mkiwa wizara mmekuta mkoa ushafanya maamuzi katika masuala ya ardhi halafu watu kwa interest zao wanabeba mgogoro kwa masahi yao ni lazima mrudi kwa mkoa kuuliza mazingira aliyo amua kutoa uamuzi huo'' alisema Makalla.